MAKAMU wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi ametembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) katika Maonesho ya 33 ya Nanenane na kujionea mchango wa benki hiyo katika kuimarisha uzalishaji wa kilimo, kuongeza thamani ya mazao na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Akiwa ameambatana na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, Makamu wa Rais alipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipango, Ushauri na Mahusiano ya Taasisi wa TADB, Mkani Waziri, ambaye alisema benki hiyo imeendelea kutoa mikopo na huduma mbalimbali za kifedha zinazowawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji kuongeza uzalishaji, tija na usalama wa chakula nchini.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Kula cha Trolle Meesle, Daniel Amulike, ameeleza namna ufadhili wa TADB ulivyowezesha kampuni yake kujenga kiwanda cha kisasa na kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula kwa kiwango kikubwa.
"Baada ya kufadhiliwa na TADB, tumetoka kuzalisha tani 30 kwa mwezi hadi kufikia tani 624 za mafuta safi ya kula kwa mwezi kupitia kiwanda cha kisasa," amesema Amulike.
Ameongeza kuwa ongezeko hilo la uzalishaji limeongeza uwezo wa kampuni kununua mazao kutoka kwa wakulima, kuimarisha soko la mazao ya mafuta na kuchangia kupunguza utegemezi wa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta pamoja na kuimarisha uwekezaji katika viwanda vya uchakataji ili kufikia lengo la kujitosheleza kwa mafuta ya kula nchini.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za kifedha kama TADB una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa kilimo, kuongeza thamani ya mazao na kufungua fursa zaidi za ajira na maendeleo kwa wananchi.
Ziara ya Makamu wa Rais katika banda la TADB imeonyesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha sekta ya kilimo kupitia uwekezaji, upatikanaji wa mitaji na maendeleo ya viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya ndani.








Comments
Post a Comment