Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema chuo hicho kimetekeleza miradi 27 ya maendeleo yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 15.66 katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuimarisha huduma kwa wanafunzi na watumishi pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa jamii.Prof. Mwegoha alisema miradi hiyo imetekelezwa katika Kampasi Kuu ya Morogoro pamoja na kampasi za Dar es Salaam na Mbeya kwa kutumia fedha za ndani, ruzuku ya Serikali na michango ya wadau wa maendeleo. Alieleza kuwa uwekezaji huo unalenga kuongeza ubora wa elimu na kukidhi ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na chuo kila mwaka.
Alitaja baadhi ya miradi iliyokamilika kuwa ni ujenzi wa majengo ya taaluma na utawala, madarasa janja, studio ya kisasa ya multimedia, ukarabati wa mabweni ya wanafunzi, ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, ujenzi wa barabara za ndani, uchimbaji wa visima vya maji, uwekaji wa taa za nishati ya jua na kamera za usalama (CCTV), pamoja na kuimarisha miundombinu ya TEHAMA kwa kuongeza uwezo wa mtandao katika kampasi zote tatu.
Aidha, Prof. Mwegoha amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 chuo kimepanga kutekeleza miradi mipya yenye thamani ya shilingi bilioni 4.83, ikiwemo kukamilisha miradi inayoendelea, kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali, kuimarisha huduma za afya, kuongeza vifaa vya TEHAMA, kufanya tafiti za kisayansi na kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi.
Pia amesema Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuimarisha matumizi ya TEHAMA na tayari kimejijengea sifa ya kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza nchini katika maendeleo na usimamizi wa mifumo ya kidijitali inayotumiwa na taasisi mbalimbali za umma. Hatua hiyo, alisema, itaendelea kuimarisha ubora wa elimu, utafiti na huduma kwa jamii sambamba na kuchangia maendeleo ya taifa.



Comments
Post a Comment