MBUNGE wa Jimbo la Tarime Mjini, Mhe. Esther Matiko, ametekeleza ahadi yake kwa Chama cha Madereva wa Pikipiki (Bodaboda) Tarime Mjini baada ya kukabidhi msaada wa shilingi milioni moja (Tsh 1,000,000) pamoja na kompyuta moja, hatua inayolenga kuimarisha utendaji na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wanachama wa chama hicho.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mhe. Matiko alisema kuwa uwezeshaji huo ni sehemu ya dhamira yake ya kuunga mkono makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi ili yaweze kujijengea uwezo na kuongeza tija katika shughuli zao za kila siku.
Ameeleza kuwa kompyuta hiyo itasaidia kurahisisha shughuli za kiutawala, utunzaji wa kumbukumbu na mawasiliano ndani ya chama, huku fedha hizo zikitarajiwa kusaidia uendeshaji wa shughuli mbalimbali za chama.
"Bodaboda ni kundi muhimu katika kukuza uchumi na kutoa huduma za usafiri kwa wananchi. Ni wajibu wetu kuwaunga mkono ili waweze kufanya kazi katika mazingira bora na yenye tija zaidi," amesema Mhe. Matiko.
Pia amewataka madereva hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, pamoja na kudumisha umoja na ushirikiano ili kujenga taswira nzuri ya taaluma yao na kuchangia maendeleo ya Tarime Mjini.
Kwa upande wao, viongozi wa Chama cha Madereva wa Bodaboda Tarime Mjini walimpongeza Mhe. Matiko kwa kutimiza ahadi yake, wakisema msaada huo utaleta mabadiliko chanya katika uendeshaji wa shughuli za chama na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wanachama.
Walieleza kuwa kitendo cha kutekeleza ahadi hiyo kinaonyesha kujali na kuthamini mchango wa madereva wa bodaboda katika maendeleo ya jamii, huku wakiahidi kuutumia msaada huo kwa malengo yaliyokusudiwa kwa manufaa ya wanachama wote.




Comments
Post a Comment