HALMASHAURI 39 ZAANZA KUHOJIWA NA LAAC KWA HOJA ZA CAG
MWENYEKITI wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),Mhe. Ado Shaibu Ado, amesema kamati hiyo imeanza zoezi la kuwahoji viongozi wa 39 kutoka mikoa 15 nchini kuhusu hoja mbalimbali zilizoibuliwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Bungeni Jijini Dodoma Ado amesema zoezi hilo linafanyika kwa niaba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likiwa na lengo la kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma katika mamlaka za serikali za mitaa.
"Kamati ya LAAC inapata nafasi ya kuwahoji wakurugenzi wa halmashauri pamoja na menejimenti zao kuhusu masuala mbalimbali yaliyoibuliwa na CAG, lakini pia tunafuatilia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na kamati katika vikao vya awali na yale yaliyotolewa na CAG," amesema.
Ameeleza kuwa Spika wa Bunge alitoa kibali kwa kamati hiyo kuendelea na zoezi hilo baada ya hatua ya awali iliyofanyika wakati wa Bunge la Bajeti, ambapo halmashauri nane zilihojiwa, huku awamu ya sasa ikihusisha halmashauri 39.
Mje. Ado amesema majukumu ya Kamati ya LAAC, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, ni pamoja na kuchunguza matumizi mabaya ya fedha za serikali za mitaa yaliyoainishwa na CAG, kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya kamati na kutoa ushauri kwa serikali ili kuimarisha usimamizi wa fedha za umma.
"Baada ya kuzikamilisha hojaji kwa halmashauri zote, tutawasilisha mapendekezo yetu bungeni ambapo yatajadiliwa na baadaye Bunge litatoa maazimio yatakayokuwa maagizo kwa Serikali," amefafanua.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, kamati ilianza kazi Agosti 3 kwa kuzihoji Halmashauri ya Manispaa ya Singida na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Agosti 4 inahoji Halmashauri ya Mji Kasulu, Manispaa ya Kigoma na Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
Ratiba hiyo itaendelea kwa mikoa ya Tabora, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Shinyanga na Manyara hadi Agosti 12, 2026.
Ado amesema hatua hiyo inalenga kutekeleza maelekezo ya Spika wa Bunge ya kuhakikisha Bunge linasimamia kikamilifu matumizi ya fedha za umma na kuongeza uwajibikaji katika serikali za mitaa kwa maslahi ya wananchi.





Comments
Post a Comment