MBUNGE wa Jimbo la Rorya, Mhe. Jafari Wambura Chege (JW-Chege), ametangaza mpango mkubwa wa kujenga na kukarabati ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata zote zenye uhitaji ndani ya jimbo hilo, hatua inayotajwa kuwa itaimarisha utendaji wa chama na kuboresha mazingira ya kazi kwa viongozi na watendaji wake.
Mpango huo umetangazwa wakati wa kikao cha Halmashauri ya CCM Wilaya ya Rorya, ambapo Mhe. Chege alisema dhamira yake ni kuhakikisha chama kinakuwa na miundombinu bora kuanzia ngazi ya wilaya, kata hadi matawi, ili kuendana na kasi ya maendeleo na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wanachama na wananchi.
Katika kuonyesha utekelezaji wa ahadi hiyo, Mbunge huyo ametoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Ofisi mpya ya CCM Wilaya ya Rorya, huku akieleza kuwa watendaji wa chama wanatarajiwa kuhamia katika jengo hilo ndani ya mwezi Agosti mwaka huu.
Mbali na kukamilisha jengo la ofisi za wilaya, Mhe. Chege ameagiza kufanyika kwa upimaji wa eneo na uchoraji wa ramani za ujenzi wa ukumbi wa kisasa utakaojengwa katika eneo hilo. Ukumbi huo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wajumbe 300 na kutumika kwa mikutano mikubwa, semina pamoja na shughuli nyingine za chama.
Akizungumza na wajumbe wa kikao hicho, Mhe. Chege amesema hatua inayofuata baada ya kukamilisha ofisi za kata ni kuanza ujenzi wa ofisi za matawi, akisisitiza kuwa lengo lake ni kuhakikisha kila ngazi ya CCM ndani ya Jimbo la Rorya inafanya kazi katika mazingira yanayostahili.
"Tunataka kujenga chama chenye misingi imara. Hilo haliwezekani bila kuwa na miundombinu bora itakayowapa viongozi na watendaji mazingira mazuri ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi," amesisitiza.
Mhe. Chege, ambaye ni mtaalamu wa ramani za ujenzi na mtumishi wa zamani wa Wizara ya Ardhi, amesema atatumia uzoefu wake kuhakikisha miradi yote ya ujenzi inatekelezwa kwa ubora, kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na matumizi sahihi ya rasilimali.
Viongozi na wanachama wa CCM wilayani Rorya wameeleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema utaimarisha shughuli za chama, kuongeza morali ya watendaji na kuacha urithi wa miundombinu utakaonufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Mpango huo unadhihirisha dhamira ya Mbunge huyo ya kuendelea kuijenga CCM kwa vitendo, sambamba na kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya Jimbo la Rorya kupitia uwekezaji katika miundombinu ya taasisi za chama.

Comments
Post a Comment