Kutokana na baadhi ya wafanyabiashara nchini kutumia vipimo visivyo sahihi katika kuwahudumia wananchi, Wakala wa Vipimo Nchini (WMA) umewaonya wafanyabiashara wanaotumia vipimo visivyokidhi viwango kuwa wanakabiliwa na adhabu kali kwa mujibu wa sheria, ikiwemo faini na kifungo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 18, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, Mtumba jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa wakala wa vipimo nchini (WMA), Alban Kihulla, amesema mtuhumiwa anayekubali kosa anaweza kutozwa faini ya Shilingi 100,000 hadi milioni 20 kwa kosa moja.
Amesema kwa anayekataa kosa na kupatikana na hatia mahakamani, adhabu ni faini ya Shilingi 300,000 hadi milioni 50, au faini pamoja na kifungo kisichozidi miaka miwili.
Kwa mkosaji wa mara kwa mara, amesema faini inaweza kufikia Shilingi milioni 100 kwa kosa moja, hatua inayolenga kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia vipimo sahihi na kulinda haki za walaji.
Kihulla amewataka wafanyabiashara na wakulima kuachana na matumizi ya magunia, madebe, makopo, mafungu na vipimo vingine visivyo rasmi katika biashara ya mazao, akisisitiza matumizi ya mizani kwa kuwa kilo ndiyo kipimo kinachotambulika katika biashara.
“Madebe, makopo, visado na mafungu siyo vipimo, wafanyabiashara tumieni mizani,” amesisitiza Kihulla, akieleza kuwa WMA inahakikisha kilo moja inakuwa kilo moja na vipimo vyote vinazingatia viwango vinavyotambulika.
Amesema matumizi ya vipimo visivyo rasmi yanaweza kusababisha kutokuwepo kwa usawa katika biashara, hivyo wananchi wanapaswa kudai kupimiwa bidhaa kwa mizani ili kuhakikisha wanapata kiasi halisi wanacholipia.
Aidha, Kihulla amesema WMA haisimamii vipimo vya bidhaa pekee, bali inahakikisha usahihi wa vipimo katika sekta mbalimbali kwa mujibu wa sheria za kitaifa, kikanda na kimataifa.
Ametoa mfano wa sekta ya afya, ambapo vipimo vya uzito huhakikiwa ili kuhakikisha mgonjwa anapata uzito halisi, jambo linalomsaidia daktari kuamua kiwango sahihi cha dawa kulingana na uzito wa mgonjwa.
Kihulla amewataka wananchi kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya matumizi ya vipimo visivyo sahihi kwa kutoa taarifa wanapobaini au kuhisi kuwa vipimo vinavyotumika si sahihi, kupitia namba 08001197, ili WMA ichukue hatua stahiki.





Comments
Post a Comment