Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe, amesisitiza kuwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 itaendelea kufanyika Tanzania, Kenya na Uganda, akikanusha taarifa na madai yanayodai kuwa mashindano hayo yanaweza kuhamishiwa katika nchi nyingine.
Dkt. Motsepe ameyasema hayo leo, Septemba 17, 2026, mara baada ya kuwasili Tanzania kwa ajili ya kukagua maendeleo ya maandalizi ya mashindano hayo, ambayo Tanzania, Kenya na Uganda zimepewa dhamana ya kuwa wenyeji.
Amesema amekuwa akisikia taarifa mbalimbali zinazodai kuwa CAF inaweza kuanza kufikiria mpango mbadala wa kuhamishia AFCON 2027 katika nchi nyingine, akisisitiza kuwa hilo halitatokea.
“Baadhi ya watu, kutokana na yale ambayo tayari yameripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari barani Afrika na sehemu nyingine duniani, wanasema Rais wa CAF anapaswa kuanza kufikiria mpango B na mpango C na kuiondoa AFCON Tanzania, Kenya na Uganda, hilo halitatokea,” amesema Motsepe.
Aidha, Rais huyo wa CAF amesema anajivunia kazi inayoendelea Tanzania katika maandalizi ya mashindano hayo, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa maandalizi katika kipindi cha miezi tisa iliyosalia kabla ya kuanza kwa AFCON 2027.
“Tupo hapa kufanya kazi pamoja, kusaidia na kutoa ushirikiano, hii ni AFCON yetu,” amesema Motsepe.















Comments
Post a Comment