BODI ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imewapa siku 30 wataalamu wote waliosajiliwa ambao wana madeni ya ada ya mwaka kuhakikisha wanalipa, ikionya kuwa watakaoshindwa kutekeleza agizo hilo wanaweza kufutiwa usajili na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Agizo hilo limetolewa leo Septemba 14, 2026 na Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ulipaji wa ada ya mwaka ya wanachama wa Bodi hiyo.
Amesema ulipaji wa ada ya mwaka ni wajibu wa kisheria kwa kila mtaalamu aliyesajiliwa na PSPTB, kwa mujibu wa Sheria ya PSPTB, Sura ya 179 ya Sheria za Tanzania, pamoja na kanuni zinazosimamia taaluma hiyo.
Mbanyi amesema kuwa mtaalamu anayeshindwa kulipa ada kwa kipindi cha miezi 24 mfululizo atachukuliwa kuwa amepoteza hadhi ya usajili na jina lake linaweza kuondolewa katika daftari rasmi la wataalamu waliosajiliwa na Bodi.
Bodi pia imeonya kuwa mtu ambaye ataendelea kufanya kazi, kujitambulisha au kujihusisha na taaluma ya ununuzi na ugavi bila kuwa amesajiliwa na PSPTB atakuwa ametenda kosa la jinai na anaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
"Endapo wataalamu wenye madeni hawatalipa ndani ya siku 30 tangu tarehe ya kutolewa kwa taarifa hiyo, hatua zaidi za kisheria na kinidhamu zinaweza kuchukuliwa dhidi yao, ikiwemo kufunguliwa mashitaka". Amesisitiza
Aidha, Mbanyi amesema majina ya watakaofutiwa usajili yatachapishwa kwenye tovuti ya PSPTB na Gazeti la Serikali kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
PSPTB ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Fedha yenye jukumu la kusimamia na kudhibiti viwango, mwenendo na maadili ya taaluma ya ununuzi na ugavi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.




Comments
Post a Comment