Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, imewaonya wananchi dhidi ya taarifa za uongo zinazotengenezwa kwa muonekano wa taarifa rasmi na kusambazwa mitandaoni, huku zikidaiwa kutolewa na Ikulu au kuhusishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika taarifa yake kwa umma, Kurugenzi hiyo imesema imebaini kuwepo kwa taarifa hizo ambazo zinatumia jina, nembo na utambulisho unaoweza kuwafanya wananchi kuamini kuwa zimetolewa rasmi na Ikulu.
Kurugenzi imeeleza kuwa taarifa zote rasmi zinazohusu shughuli za Mheshimiwa Rais hutolewa kupitia Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, na wananchi wanapaswa kuzihakiki kupitia vyanzo rasmi kabla ya kuzipokea au kuzisambaza.
Vyanzo rasmi vilivyotajwa ni pamoja na ukurasa wa Instagram wa Ikulu Tanzania (@ikulu_mawasiliano), Facebook wa Ikulu Tanzania (@ikulu.mawasiliano) pamoja na tovuti rasmi ya Ikulu.
Aidha, Kurugenzi imewakumbusha wananchi kuwa utengenezaji na usambazaji wa taarifa za uongo kwa kutumia jina, nembo au utambulisho wa Rais au Ikulu ni kosa kisheria, kwa mujibu wa Kifungu cha 15 na 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sura ya 443.
Kurugenzi imewataka wananchi kuwa makini na taarifa wanazokutana nazo kwenye mitandao ya kijamii na kuhakikisha wanazithibitisha kupitia vyanzo rasmi kabla ya kuzisambaza kwa wengine.
Taarifa hiyo imetolewa na Bakari S. Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Comments
Post a Comment