Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), John Wambura Bina, leo Septemba 8, 2026, amefika Kizimkazi, Zanzibar, nyumbani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenda kumpa pole kufuatia kifo cha mama mzazi wa Rais, Mzee Hafidh Ameir.
Mzee Hafidh Ameir alifariki dunia jana, Septemba 7, 2026, na kuzikwa leo katika eneo la Kizimkazi, Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Rais wa FEMATA ameambatana na Makamu wa Rais wa FEMATA, Victor Michael Tesha, Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Mkoa wa Geita, Charles Titus Kabuo, pamoja na Mama Sara Masasi, mmoja wa wamiliki wa kiwanda cha kusafisha dhahabu nchini.
Viongozi hao wametoa salamu za pole kwa Rais Samia, familia na ndugu wa marehemu, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu, faraja na uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
Rais wa FEMATA amesema wamefika Kizimkazi kwa ajili ya kuonesha upendo, mshikamano na umoja wenye utu kwa Rais Samia na familia yake katika kipindi hiki cha majonzi.
Amesema ziara hiyo pia ni ishara ya mshikamano wa wachimbaji wadogo wa madini na uongozi wa nchi, akitambua mchango wa Serikali katika kuendeleza sekta ya madini na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
Aidha, viongozi hao wameendelea kutoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote walioguswa na msiba huo, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu amrehemu marehemu Hafidh Ameir, ampe pumziko la milele na kuijaza familia yake nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.





Comments
Post a Comment