Skip to main content

@marato_tv

@marato_tv
#sauti_ya_jamii

MAHAKAMA KUU YAPANGA KIKAO CHA AWALI CHA SHAURI LA UHAINI LA LISSU


 Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imepanga kufanya kikao cha awali cha maandalizi ya usikilizwaji wa Shauri la Uhaini Na. 19605/2025 linalomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Antiphas Lissu.

Kwa mujibu wa waraka rasmi uliotolewa Julai 31, 2026 na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, H. S. Mushi, kikao hicho cha awali (Pre-Session Meeting) kitafanyika Agosti 5, 2026 kuanzia saa nane kamili mchana kwa njia ya mtandao kupitia Masjala Ndogo ya Mahakama Kuu, Dar es Salaam.

Mahakama imeeleza kuwa lengo la kikao hicho ni kujadili maandalizi muhimu yatakayowezesha usikilizwaji wa shauri hilo kufanyika kwa ufanisi kabla ya kuanza rasmi kwa mwenendo wa kesi.

Aidha, usikilizwaji wa shauri hilo umepangwa kuanza Agosti 10, 2026 na unatarajiwa kuendelea hadi Septemba 7, 2026, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Mahakama.

Waraka huo umeelekezwa kwa Mkuu wa Mashtaka wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Gereza Kuu la Ukonga na mshtakiwa Tundu Antiphas Lissu, huku nakala zikitumwa kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mtendaji wa Mahakama pamoja na Wakili Hekima Mwasipu anayewakilisha jopo la mawakili wa utetezi.



Mahakama imezitaka pande zote zinazohusika kuzingatia muda uliopangwa wa kikao hicho, ikisisitiza kuwa maandalizi ya awali ni sehemu muhimu ya kuhakikisha shauri linaendelea kwa utaratibu na kwa kuzingatia misingi ya haki na sheria.

Comments