Arusha.
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeanza utekelezaji wa mpango wa kuchimba visima 67,000 kwa wakulima wadogo nchini, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao, kuimarisha usalama wa chakula na kufungua maelfu ya ajira kwa vijana.
Akizungumza katika Kongamano la 10 la Ununuzi wa Umma mwaka 2026 jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amesema mpango huo unatekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa mradi wa uchimbaji wa visima kwa wakulima wadogo katika Maonesho ya Nanenane yaliyofanyika Mbeya mwaka 2023.
«"Lengo letu ni kumkomboa mkulima mdogo kutokana na utegemezi wa mvua kwa kuhakikisha anapata maji ya uhakika kwa ajili ya uzalishaji wa mwaka mzima. Hii itachochea uzalishaji, kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini," amesema Mndolwa.»
Amesema mpango huo pia unalenga kufikisha huduma za umwagiliaji kwa wakulima walio nje ya skimu rasmi za umwagiliaji ili kuwapa fursa sawa ya kuzalisha kwa tija.
Kwa mujibu wa Mndolwa, utekelezaji wa mradi huo utafungua ajira kati ya vijana 2,000 na 4,000 kupitia shughuli za uchimbaji wa visima, ufungaji wa pampu na usimamizi wa mifumo ya umwagiliaji.
«"Kupitia mpango huu tunawajengea vijana ujuzi na kuwapa ajira katika sekta ya umwagiliaji. Tunataka vijana wawe sehemu ya suluhisho la kuongeza uzalishaji wa kilimo nchini," amesema.»
Ameeleza kuwa Serikali inatoa ruzuku katika uchimbaji wa visima na ununuzi wa pampu za kusukuma maji ili kuwawezesha wakulima kumudu gharama za uwekezaji huo.
Kila kisima kinatarajiwa kuhudumia wastani wa wakulima 16 na kumwagilia hadi ekari 40, huku utambuzi wa maeneo ya utekelezaji ukifanyika kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya.
Akitoa tathmini ya utekelezaji wa mradi huo, Mndolwa amesema visima 390 tayari vimechimbwa katika mikoa 15 nchini, wakati Serikali imenunua pampu 2,000, ambapo pampu 1,000 tayari zimepokelewa na kusambazwa katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Kigoma, Simiyu, Geita na Katavi.
«"Mpaka sasa wakulima 15,022 wamenufaika na mpango huu kupitia vikundi 769. Miongoni mwao wanawake ni 6,335 na wanaume ni 8,702, huku zaidi ya ekari 13,518 zikitarajiwa kumwagiliwa katika hatua ya awali," amesema.»
Mbali na mpango wa visima, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kutekeleza miradi 146 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji pamoja na miradi 634 ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu na mabwawa ya umwagiliaji nchini.
Mndolwa amesema mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo yanatokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali, wakiwemo Halmashauri 184 nchini, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) pamoja na vyuo vya ufundi vinavyoendelea kuandaa wataalamu watakaotekeleza miradi hiyo.






Comments
Post a Comment