Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha sekta ya kilimo zimeendelea kuzaa matunda baada ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuongeza mtaji wake kutoka Shilingi bilioni 60 hadi kufikia Shilingi bilioni 452.16, hatua inayoongeza uwezo wa benki hiyo kufadhili kilimo, mifugo na uvuvi kwa kiwango kikubwa zaidi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 30, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya kilimo Tanzania TADB, Frank Nyabundege, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali pamoja na ushirikiano na taasisi mbalimbali za maendeleo.
Amesema kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita, mtaji wa TADB ulikuwa Shilingi bilioni 60 pekee, lakini sasa umefikia Shilingi bilioni 452.16, jambo linaloifanya benki hiyo kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.
"Kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita, mtaji wa TADB ulikuwa Shilingi bilioni 60 pekee. Leo umefikia Shilingi bilioni 452.16, jambo linalotupa uwezo mkubwa zaidi wa kuwahudumia wakulima, wafugaji na wavuvi," amesema Nyabundege.
Amefafanua kuwa mwaka 2021 Serikali iliongeza mtaji wa Shilingi bilioni 208, mwaka 2024 ukaongezwa tena kwa Shilingi bilioni 174.16 kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), huku mwaka 2025 Serikali ikiongeza Shilingi bilioni 10 na kufikisha kiwango cha sasa.
Mbali na ongezeko hilo la mtaji, TADB imefanikiwa kuvutia zaidi ya Shilingi bilioni 590 kutoka kwa washirika wa maendeleo, Mfuko wa Dhamana (SCGS) pamoja na Serikali, hatua iliyoongeza uwezo wa benki hiyo kufadhili miradi ya kisasa ya kilimo na kuongeza tija katika uzalishaji.
Nyabundege amesema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 73.6 ya mikopo yote iliyotolewa na TADB katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ilitolewa kati ya mwaka 2022 na 2025, ishara ya kasi ya uwekezaji na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kifedha katika sekta ya kilimo.
Amesema benki hiyo itaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuongeza uwekezaji katika kilimo, mifugo na uvuvi, kuimarisha minyororo ya thamani, kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa, kuwawezesha vijana na wanawake, pamoja na kufadhili miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, ametangaza kuwa TADB ni Mdhamini Mkuu wa Maonesho ya 88 ya Nane Nane mwaka 2026 na kuwakaribisha wananchi kutembelea banda la benki hiyo ili kujionea huduma, bidhaa na fursa mbalimbali za kifedha zinazotolewa kwa wadau wa sekta ya kilimo.
"Kilimo kinabenkika, na tutaendelea kushirikiana na Serikali na wadau kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa chachu ya ajira, usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi wa Taifa," amesisitiza Nyabundege.
TADB ni benki ya Serikali iliyoanzishwa kuwezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata huduma za kifedha.


Comments
Post a Comment