WATOTO nchini wametaka Serikali kuimarisha utekelezaji wa sheria na sera zinazolinda haki zao, wakisisitiza kukomeshwa kwa vitendo vya ukatili ikiwemo kupigwa viboko shuleni na ndoa za utotoni, wakieleza kuwa hali hizo zinaweza kuathiri elimu, ustawi na mustakabali wao.
Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 11, 2026, na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto, Daniel Magembe, kwa niaba ya watoto nchini, katika kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya watoto.
Magembe amesema pamoja na kuwepo kwa taratibu zinazodhibiti matumizi ya viboko shuleni, bado baadhi ya walimu wanaendelea kutumia adhabu hiyo kwa kiwango kikubwa, wakiamini kuwa ndiyo njia sahihi ya kurekebisha tabia za wanafunzi.
Amesema matumizi ya viboko yanaweza kuwafanya baadhi ya wanafunzi kuishi kwa hofu, kupoteza kujiamini na kushindwa kushiriki kikamilifu katika masomo, hivyo Serikali na wadau wanapaswa kutafuta njia mbadala za kujenga nidhamu bila kumuweka mtoto katika mazingira ya ukatili.
“Tunataka suala la viboko shuleni liangaliwe kwa umakini. Viboko ni sehemu ya ukatili na vinajenga hofu na kutokujiamini kwa wanafunzi. Kuna njia nyingine za kumsaidia mtoto kubadilika kitabia bila kutumia adhabu inayoweza kumuathiri,” amesema Magembe.
Amesema baadhi ya shule ambazo zimepunguza au kuacha matumizi ya viboko bado zimeendelea kuwa na wanafunzi wanaofanya vizuri kitaaluma na kitabia, akitaka uzoefu huo uzingatiwe katika kuboresha mifumo ya malezi na nidhamu shuleni.
Katika suala la ndoa za utotoni, Magembe amesema watoto wameitaka Serikali kuendelea kufanya maboresho katika sheria na kuimarisha utekelezaji wa mikakati ya kuwalinda watoto dhidi ya kuingia kwenye ndoa wakiwa katika umri mdogo.
Amesema baadhi ya watoto bado wanakabiliwa na mazingira yanayoweza kuwafanya waingie kwenye ndoa kabla ya kukamilisha masomo na kujenga msingi wa maisha yao, jambo linaloweza kuathiri elimu na fursa zao za baadaye.
“Watoto wanataka kusoma na kujenga maisha yao, lakini kuna mazingira ambayo yanawafanya waingie kwenye ndoa wakiwa bado wadogo. Serikali iendelee kutoa elimu na kuweka mikakati maalumu katika maeneo ambayo tatizo la ndoa za utotoni bado ni kubwa,” amesema.
Aidha, amesema watoto wameitaka Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia, hususan maeneo ya vijijini ambako baadhi ya shule bado zinakabiliwa na changamoto za miundombinu, ikiwemo ukosefu wa vyumba vya madarasa na mazingira magumu ya kufikika.
Magembe amesema ujenzi wa shule, madarasa na miundombinu mingine ya elimu ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa ya elimu bila kujali wanaishi mijini au vijijini.
Amesema watoto wanaamini kuwa uwekezaji katika elimu, mazingira salama ya kujifunzia na ulinzi dhidi ya aina zote za ukatili ni msingi wa kuwawezesha kutimiza ndoto zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Kamati Kuu ya Baraza la watoto la Taifa, imekutana kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu watoto pamoja na kujengewa uwezo kuhusu Sera, sheria na miongozo inayotekelezwa na Serikali pamoja na wadau kuhakikisha haki za watoto zinalindwa.



Comments
Post a Comment