Na Mwanamkuu Mwandoro, Tanga.
Kampuni ya bima ya BUMACO imewataka wateja wake kuhakikisha wanauhisha bima zao mara tu zinapoisha muda wake ili kuweza kupata msaada wa haraka pale wanapopata changamoto.
Wito huo umetolewa na Afisa Masoko wa kampuni hiyo Mkoa wa Tanga Hosea Urasa wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo amesema kuwa changamoto inaweza kutokea wakati wowote ule hivyo ni vyema wadau wao ikiwemo wamiliki wa vyombo vya moto na nyumba wakawa tayari muda wote.
Urasa amesema kwasasa mwitiko ni mkubwa Kwa wakazi wa Tanga tofauti na awali katika kukata bima na hii imechagizwa na elimu wanayoitoa kwa jamii juu ya umuhimu wa kuwa na bima na hasa ukataji wa bima za moto.
"Watu wa Tanga ni waelewa wanachohitji ni kupatiwa elimu tu,hata baada ya lile janga la moto lililotokea stendi ya daladala baada ya kutoa elimu muitikio umeongezeka zaidi," alisema urasa
Aidha Urasa ameongeza kuwa BUMACO wanatoa bima za maisha,mali, vyombo vya moto (magari,pikipiki,mitambo kwaajili ya ukandarasi) pamoja na bima za moto (nyumba ya kuishi,vituo vya mafuta,magodaun,sehemu za biashara).
Pia kuna bima ya marine ambayo imekuwa na mwitikio mkubwa sana kutokana na upanuzi wa bandari na bima hii inahusika na vyombo vya usafiri vya majini,mizigo inayosafirishwa kupitia majini.
"Kupitia bandari ya Tanga BUMACO tumepata fursa nyingi sana ,Kuna watu wanaokuja kukata bima za mizigo pamoja na magari yao", Urasa.
Urasa ameiomba serikali kuendelea kuwekeza nguvu Kwa katika bandari ya Tanga na kuzidi kufungua fursa katika mkoa wa Tanga na Tanzania Kwa ujumla kwani bandari hii imekuwa ikihudumia mpaka nchi jirani Kama vile Kenya, Malawi.
Urasa alimalizia kwa kuwataka wananchi kutoa taarika Kwa haraka yaani kufikisha taarifa na nyaraka husika kwa wakati pindi wanapofikwa na majanga ili kuwahi kupatiwa stahiki zao.

Comments
Post a Comment