TANESCO: BAADHI YA MIKOA KUKOSA UMEME KWA MUDA KUPISHA UKAMILISHAJI WA MRADI WA 400KV CHALINZE–DODOMA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limetangaza kuwa baadhi ya mikoa nchini itakumbwa na kukosekana kwa huduma ya umeme kwa muda katika kipindi cha kuanzia Julai 30 hadi Agosti 17, 2026, ili kupisha utekelezaji wa hatua za mwisho za Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowele, amesema mradi huo umefikia asilimia 94 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika rasmi Agosti 21, 2026.
Amesema hatua zilizobaki zinahusisha kazi ya kuvuta nyaya za umeme katika maeneo ya Mkambalani mkoani Morogoro na Kikombo mkoani Dodoma, kazi inayohitaji baadhi ya njia za kusafirisha umeme kuzimwa kwa muda ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi, wananchi pamoja na miundombinu ya umeme wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
"Kazi hizi ni muhimu kwa ajili ya kukamilisha mradi huu wa kimkakati, hivyo kutakuwa na ulazima wa kusitisha huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo kwa muda kulingana na ratiba itakayopangwa," amesema Gowele.
Kwa mujibu wa TANESCO, awamu ya kwanza ya utekelezaji itaanza Julai 30 hadi Agosti 4, 2026 katika eneo la Mkambalani, Morogoro, huku awamu ya pili ikifanyika kuanzia Agosti 11 hadi 17, 2026 katika eneo la Kikombo, Dodoma.
Gowele ameeleza kuwa katika kipindi hicho huduma ya umeme inaweza kukosekana kati ya saa 12:00 asubuhi na saa 11:00 jioni katika siku na maeneo tofauti, akisisitiza kuwa si wateja wote wataathirika kwa siku zote, bali kutakuwa na ratiba maalumu kulingana na eneo husika.
Aidha, amesema TANESCO itawafahamisha wananchi mapema kuhusu maeneo yatakayoathirika kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii pamoja na makundi rasmi ya WhatsApp ya shirika hilo ili kuwawezesha kufanya maandalizi ya shughuli zao.
Amebainisha kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara haitaathirika na zoezi hilo, huku baadhi ya maeneo katika kanda ya kati, kaskazini, ziwa, magharibi na kusini magharibi yakitarajiwa kukumbwa na kukatika kwa umeme kwa nyakati tofauti kulingana na ratiba ya utekelezaji wa kazi.
Mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa umeme nchini, kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati ya umeme na kuboresha uwezo wa kusafirisha umeme kutoka maeneo ya uzalishaji kwenda kwa watumiaji katika sehemu mbalimbali za Tanzania.


Comments
Post a Comment