Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Mkufunzi Mkuu wa Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza, SSP Abduhaj Mkombe kwa niaba ya Mkuu wa Chuo, amesema chuo hicho ni mdau mkuu katika kuhakikisha kinapunguza vifo vitokanavyo na ajali za majini katika Ziwa Victoria na maeneo mengine nchini.
"Sisi kama Polisi tuna dhamana ya kusimamia usalama majini na kuhakikisha raia na mali zao wanakuwa salama. Tumeona ipo haja ya kushiriki kwenye tukio hili ili kuonyesha mchango wetu katika kupunguza vifo vinavyotokana na kuzama maji," amesema Mkombe.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai, amelipongeza Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama kwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kuokoa maisha ya raia na mali zao pindi ajali zinapotokea ndani ya Ziwa Victoria.
Kuhusu jitihada za Serikali kukabiliana na tatizo hilo, Mhe Ngubiagai amesema serikali imeendelea kuimarisha mikakati ya kuzuia ajali za majini na kuboresha huduma za uokoaji, ambapo taasisi muhimu ikiwemo Jeshi la Polisi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji zinafanya kazi kwa ukaribu mkubwa kuliko wakati mwingine wowote.
"Polisi Wanamaji na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na majanga yote ya majini wakati wowote," alisisitiza Mhe. Ngubiagai.
Kwa upande wake, ASP Prisca Lawei, aliyemwakilisha Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, alisema ili kuzuia vifo vitokanavyo na ajali za majini, Jeshi hilo limekuwa likitoa elimu kwa makundi yanayotumia Ziwa Victoria wakiwemo wavuvi na wananchi wanaoishi kando ya ziwa hilo ili kuwawezesha kuwa na uelewa wa kujiokoa pindi vyombo vinapopata hitilafu.
Naye, Polisi Kata wa Kata ya Nyamagana, Mkaguzi wa Polisi Luhendeka Masanja, alieleza kuwa eneo lililofanyikia maadhimisho hayo linatumika sana kwa shughuli za kiutalii na kwamba amekuwa akitoa elimu ya usafiri salama kwa wananchi na watalii wanaotembelea eneo hilo.













Comments
Post a Comment