Wananchi wa Kata ya Mwabomba, hususan Kijiji cha Mhulula wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, wamehimizwa kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya reli kwa kutambua kuwa uwekezaji huo ni mali ya Watanzania wote na una mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Rai hiyo imetolewa Julai 27, 2026 na Mkuu wa Kituo cha Polisi Reli Mkoa wa Mwanza wakati wa mkutano wa hadhara uliowakutanisha viongozi wa serikali za vijiji na kata, wataalamu kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC) pamoja na Jeshi la Polisi. Mkutano huo ulilenga kutoa elimu kuhusu ulinzi wa miundombinu ya reli, usalama wa jamii, kuzuia ukatili wa kijinsia na utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Akizungumza na wananchi, Mkuu wa Kituo cha Polisi Reli Mkoa wa Mwanza, ASP Jovitha Tibangayuka, alisema ziara hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi katika kulinda miundombinu ya reli na rasilimali nyingine za taifa.
"Jukumu la kulinda miundombinu ya reli ni la kila mwananchi. Si la Kikosi cha Polisi Reli au Shirika la Reli Tanzania (TRC) pekee. Mtu yeyote atakayebaini vitendo vya wizi wa vyuma vya reli, uharibifu wa uzio au miundombinu mingine, atoe taarifa mara moja kwa vyombo vya usalama ili hatua za kisheria zichukuliwe," alisema ASP Tibangayuka.
Aidha, aliwataka wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa mapema badala ya kufumbia macho vitendo hivyo, akisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni nguzo muhimu katika kuzuia uhalifu.
Kwa upande wake, Afisa wa Kitengo cha Mazingira na Jamii kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), James Zacharia, alitoa elimu ya usalama kwa watumiaji wa reli, akisisitiza umuhimu wa kuvuka njia za treni katika maeneo rasmi yaliyowekwa alama ili kuepusha ajali.
"Wananchi wanapaswa kutumia vivuko rasmi vya reli vilivyotengwa kwa ajili ya usalama wao. Kuvuka kiholela kunaweza kuhatarisha maisha," alisema Zacharia.
Naye Polisi Kata wa Mwabomba, A/Insp Paschal Darabe, aliwahimiza wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi wanapowakamata watuhumiwa wa makosa mbalimbali. Aliwataka kuwafikisha watuhumiwa hao katika vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake, huku akisisitiza matumizi ya njia za amani na za kisheria katika kutatua migogoro ya ardhi.
Wananchi walioshiriki mkutano huo walieleza kuridhishwa na elimu waliyoipata na kuahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na TRC katika kulinda miundombinu ya reli na kudhibiti vitendo vya uhalifu.
"Sisi kama wananchi wa Mhulula tumeipokea vizuri elimu hii na tunaahidi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na vitendo vyote vinavyohatarisha usalama wa reli," alisema Emmanuel Silvester, mkazi wa Kijiji cha Mhulula.
Naye Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Mhulula, Bi. Marietta Shija, aliwahimiza wananchi kutoruhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia kuendelea kimya kimya.
"Ukiona mtu anafanyiwa ukatili usinyamaze. Toa taarifa mapema kwa viongozi wa kijiji, Sungusungu au vyombo vya usalama ili hatua zichukuliwe," alisema.
Mkutano huo ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi na Shirika la Reli Tanzania za kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya reli, kuimarisha usalama wa wananchi na kukuza ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya ulinzi na usalama.











Comments
Post a Comment