Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini na mzazi wa mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mwita Waitara, amelipongeza Jeshi hilo kwa kuendelea kuwajenga vijana katika misingi ya uzalendo, nidhamu, uwajibikaji na kujitegemea, akisema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa katika kuwaandaa vijana kukabiliana na changamoto za maisha.
Waitara ameyasema hayo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria, Operesheni Linda Amani na vijana waliojitolea, iliyofanyika katika Kikosi cha Ruvu JKT kilichopo Mlandizi, mkoani Pwani, ambapo amesema vijana wanaomaliza mafunzo hayo wanapaswa kutumia ipasavyo maarifa na stadi walizopata ili kujiajiri, kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuwa raia wema wenye mchango kwa Taifa.
Aidha, Waitara amehimiza matumizi sahihi ya teknolojia ya Akili Bandia (AI) katika kuwaandaa vijana kwa mazingira ya sasa, akisema teknolojia hiyo inaweza kutumika kuwaongezea maarifa na stadi mbalimbali zitakazowasaidia kukabiliana na mahitaji ya dunia ya kisasa hivyo pia amewahimiza wazazi nchini kuwapa nafasi vijana wao kushiriki mafunzo ya JKT kwa kuwa yanawasaidia kujenga nidhamu, ukakamavu, uzalendo na uwezo wa kujitegemea.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Brigedia Jenerali Justus Kitaa, amesema mafunzo ya JKT yana nafasi kubwa katika kumjenga kijana wa Kitanzania kuwa mvumilivu, mwenye nidhamu, ukakamavu na uzalendo, hali inayomsaidia kutambua wajibu wake katika kulinda, kujenga na kuendeleza Taifa.
Akizungumza kama mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mipango Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa, Brigedia Jenerali Gerald Omary, amewataka wahitimu hao kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kujihusisha na vikundi vya uhalifu, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwafanya kupoteza mwelekeo na kushindwa kutimiza wajibu wao kwa Taifa.
Brigedia Jenerali Omary pia amewaasa vijana kuwa waangalifu katika matumizi ya mitandao ya kijamii na kuepuka kuitumia vibaya kwa kuwatukana, kuwakejeli au kuwadharau viongozi, akieleza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia yanaweza kuleta madhara kwa jamii na kuathiri mshikamano unaohitajika katika ujenzi wa Taifa.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Ruvu JKT, Kanali George Kazaula, amesema baadhi ya vijana hawakufanikiwa kuhitimu mafunzo hayo kutokana na utoro na utovu wa nidhamu wakati wa mafunzo, akisisitiza umuhimu wa vijana kuzingatia kanuni na taratibu za JKT ili kunufaika kikamilifu na mafunzo wanayopewa.
Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Karim amesema mafunzo ya JKT yanapaswa kupewa nafasi na vijana wengi zaidi kwa kuwa yanawapatia maarifa kuhusu nidhamu, uzalendo, utimamu wa mwili na stadi mbalimbali za kazi.
Amesema mafunzo hayo pia yanazingatia ushirikishwaji wa vijana wenye mahitaji mbalimbali, wakiwemo watu wenye ulemavu, kwa kuwapatia fursa ya kujifunza kulingana na uwezo wao.
Karim ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia vijana kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha, kufanya kazi kwa ushirikiano na kuheshimu mamlaka pamoja na jamii. Amewataka vijana wenzake kutumia maarifa na stadi walizopata JKT kwa manufaa yao, familia zao na Taifa kwa ujumla.

















Comments
Post a Comment