Dhana kwamba elimu ya ufundi stadi ni kwa watu waliokosa fursa za elimu ya juu inaendelea kupotea, huku wahitimu wenye vyeti, stashahada, shahada na hata shahada za uzamili wakijitokeza kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi ili kuongeza ujuzi na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amesema katika kipindi cha mwaka 2022/2023 hadi 2025/2026, jumla ya waombaji 794 wa mafunzo ya ufundi stadi walikuwa tayari na elimu za juu katika taaluma mbalimbali.
Amesema kati yao, 522 walikuwa na vyeti vya taaluma nyingine, 120 walikuwa na stashahada, 151 walikuwa na shahada na mmoja alikuwa na shahada ya uzamili.
Kasore ameyasema hayo leo, Septemba 4, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu nafasi ya VETA katika kujenga Taifa lenye wananchi wenye ujuzi.
Amesema ongezeko hilo linaonesha mabadiliko makubwa katika mtazamo wa jamii kuhusu elimu ya ufundi stadi, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na watu waliokosa nafasi ya kuendelea na elimu nyingine.
“Uelewa wa umma kuhusu thamani ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi unazidi kukua, huku dhana ya ufundi stadi kuwa ni kwa ajili ya kundi fulani lililokosa fursa zingine za kielimu ukizidi kupungua,” amesema Kasore.
CPA Kasore amesema sambamba na kuongezeka kwa mahitaji ya ujuzi, VETA imeendelea kuongeza nafasi za mafunzo nchini, ambapo udahili katika vyuo vinavyomilikiwa na mamlaka hiyo umeongezeka kutoka wanachuo 69,347 mwaka 2022/2023 hadi 116,468 mwaka 2025/2026.
Amesema ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuanza kwa shughuli za vyuo vipya 33 vya VETA katika ngazi za mikoa na wilaya.
"Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa vyuo vipya 65 vya VETA, ambavyo vinajumuisha vyuo 64 vya wilaya na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe". Amesema
Vyuo hivyo vinatarajiwa kuanza kutoa mafunzo Januari 2027 na vinatarajiwa kuongeza uwezo wa VETA kudahili wanafunzi wapya 130,892 katika mwaka huo.
Katika hatua nyingine, CPA Kasore amesema VETA imeendelea kurasimisha ujuzi wa mafundi waliojifunza kupitia uzoefu, uanagenzi na mazingira ya kazi bila kupitia mfumo rasmi wa mafunzo.
Kupitia Mpango wa Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (RPL), jumla ya mafundi 18,008 wamerasimishiwa ujuzi wao kupitia Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi.
Amesema katika kipindi cha 2022/2023 hadi 2025/2026, pia jumla ya mafundi 426 wenye elimu za juu waliomba kurasimishiwa ujuzi wao.
Kati yao, 82 walikuwa na vyeti vya taaluma nyingine, 167 stashahada, 170 shahada na saba shahada za uzamili.
Kwa mujibu wa Kasore, takwimu hizo zinaonesha wazi kuwa ujuzi wa ufundi stadi sasa unatambuliwa kama nyenzo muhimu ya kuongeza ushindani katika ajira na uzalishaji.
Kasore ametoa wito kwa jamii kubadili mtazamo kuhusu elimu ya ufundi stadi na kuacha kuichukulia kama chaguo la mwisho kwa mwanafunzi anayeshindwa kuendelea na elimu nyingine.
Amesema Tanzania inayolenga kujenga uchumi wa viwanda, kukuza sekta ya madini, kilimo cha kisasa, TEHAMA, ujenzi na uchumi wa buluu inahitaji mamilioni ya Watanzania wenye ujuzi wa vitendo.
“Tusimwambie mtoto wetu, ‘ukifeli shule utasoma ufundi.’ Tumwambie, ‘ukitaka kuwa na ujuzi wa kujenga maisha na kujenga Taifa, soma ufundi stadi,’” amesema.
Amesema VETA imejipanga kuongeza ubora wa mafunzo, kupanua fursa za mafunzo, kuimarisha miundombinu na vifaa, kutumia TEHAMA, kuendeleza utafiti na ubunifu pamoja na kuimarisha ushirikiano na waajiri na viwanda.
CPA Kasore amesema katika kipindi kijacho, VETA inalenga kuhakikisha ongezeko la udahili linaenda sambamba na ubora wa mafunzo, mahitaji ya waajiri pamoja na uwezo wa wahitimu kupata ajira au kujiajiri.
"Mafunzo yataelekezwa zaidi katika sekta zenye mahitaji makubwa ya nguvu kazi, ikiwemo kilimo na uchakataji wa mazao, ujenzi, madini, nishati, TEHAMA, usafiri na usafirishaji, uzalishaji viwandani na uchumi wa buluu". Amesema.
Aidha, kupitia Programu ya Elimu na Ujuzi kwa Ajira zenye Tija (ESPJ II), VETA inalenga kuimarisha miundombinu, vifaa vya kisasa, matumizi ya teknolojia za kidijitali na ujuzi wa wakufunzi.
CPA Kasore amesema lengo kuu ni kuhakikisha mfumo wa ufundi stadi unaunganisha udahili, mafunzo, umahiri, ajira au kujiajiri, tija na uzalishaji, ili wahitimu wawe sehemu muhimu ya ujenzi wa uchumi wa Taifa.
Amesisitiza kuwa safari ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 haiwezi kufanikiwa kwa kutegemea rasilimali pekee, bali inahitaji pia rasilimali watu yenye ujuzi, ubunifu, nidhamu na uwezo wa kutumia teknolojia.
“Tanzania ya viwanda inahitaji mafundi; Tanzania ya madini inahitaji mafundi; Tanzania ya TEHAMA inahitaji mafundi; Tanzania ya kilimo cha kisasa inahitaji mafundi; na Tanzania ya Dira 2050 inahitaji mamilioni ya Watanzania wenye ujuzi,” amesema Kasore.



Comments
Post a Comment