WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amefanya kikao kazi na madiwani pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na uwajibikaji katika kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kikao hicho kiliwahusisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, Ndg. Ramadhani Possy, Wakuu wa Idara, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata pamoja na madiwani, ambapo walijadili kwa kina namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vilivyowekwa na Serikali.
Akizungumza katika kikao hicho,kilichofanyika wilayani chalinze Mhe. Kikwete amesema mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanategemea kwa kiwango kikubwa utendaji wenye weledi, uwajibikaji na ushirikiano wa viongozi na watumishi katika ngazi zote za Serikali.
" Halmashauri zina nafasi muhimu ya kutafsiri dira hiyo kwa vitendo kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa wananchi". Amesisitiza Mhe. Kikwete
Aidha, kikao hicho kimetoa fursa kwa viongozi hao kubadilishana mawazo, kupitia mipango ya maendeleo na kuweka mikakati itakayoongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, usimamizi wa rasilimali za umma na utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi wa Wilaya ya Chalinze.
"Ushirikiano kati ya viongozi wa kisiasa, watumishi wa umma na wananchi ni msingi muhimu wa kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa". Amesema
Ametoa wito kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, weledi na kujituma ili kuhakikisha Chalinze inakuwa miongoni mwa halmashauri zinazoongoza katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuchangia kikamilifu katika ustawi wa Taifa.




Comments
Post a Comment