Na Mwandishi Wetu - Dodoma
Wanafunzi waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza ya udahili wa Shahada ya Kwanza sasa wamepata fursa nyingine baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kufungua Awamu ya Pili ya Udahili kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 8,2026 na Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Charles Kihampa amesema awamu hiyo itafunguliwa hadi Septemba 21, 2026, huku waombaji ambao hawakuweza kukamilisha maombi au hawakupata nafasi katika awamu ya kwanza wakitakiwa kutumia fursa hiyo kuomba katika vyuo wanavyopenda.
"Taarifa hiyo inakuja wakati ambapo idadi kubwa ya vijana imeonyesha uhitaji wa kuendelea na elimu ya juu nchini, katika awamu ya kwanza, jumla ya waombaji 149,645 waliomba kujiunga na vyuo 93 vinavyodahili wanafunzi katika Shahada ya Kwanza",amesema.
Amesema idadi ya programu za masomo zilizowasilishwa pia imeongezeka kutoka 894 mwaka 2025/2026 hadi 1,019 mwaka huu ikiwa ni sawa na ongezeko la programu 125.
"Wanafunzi zaidi ya 117,000 wamepata nafasi ambapo kati ya waombaji wote walioomba udahili katika awamu ya kwanza 117,334 sawa na asilimia 78.4 wamepata nafasi katika vyuo walivyoomba,"amesema.
Pia ameongeza kuwa, kwa wale ambao wamepata udahili katika chuo zaidi ya kimoja, TCU imewataka kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja pekee.
"Mwanafunzi aliyepata nafasi zaidi ya moja anatakiwa kuchagua chuo anachotaka kusoma na kukamilisha uthibitisho ndani ya muda uliowekwa,"amesema.

Comments
Post a Comment