RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua majengo ya Ofisi za Wizara 26, Taasisi za Serikali 11 pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1 katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Uzinduzi huo utafanyika Septemba 8, 2026 katika Uwanja wa Mashujaa, Mji wa Serikali Mtumba, ikiwa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Sept 6,2026 Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema uzinduzi huo utahusisha maeneo matatu makubwa ambayo ni majengo ya Wizara, majengo ya Taasisi za Serikali na barabara za lami zilizojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba.
Ujenzi wa Mji wa Serikali ulianza kutekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilianza Novemba 28, 2018 na kukamilika Machi 22, 2019, ikihusisha ujenzi wa majengo 23 ya ofisi za awali.
"Baadhi ya majengo mengine yaliyojengwa katika awamu hiyo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na jengo la Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), hatua iliyowezesha baadhi ya watumishi wa Serikali kuhamia Mtumba". Amesema Prof. Kabudi
Prof. Kabudi amesema Awamu ya pili ilianza Oktoba 2021, ikihusisha ujenzi wa majengo ya kudumu ya Wizara na Taasisi za Serikali pamoja na miundombinu mbalimbali, ikiwemo barabara za lami, mifumo ya mawasiliano, umeme, maji, TEHAMA na huduma za kijamii.
"Kukamilika kwa majengo hayo kutawawezesha watumishi 18,510 kufanya kazi katika ofisi za Mji wa Serikali Mtumba". Amesema
Aidha, Prof. Kabudi amesema Ujenzi wa majengo hayo umehusisha wakandarasi 11, ambapo watano ni taasisi za Serikali na sita ni kampuni kutoka sekta binafsi, huku washauri elekezi watano wote wakiwa taasisi za Serikali.
"Taasisi zilizohusika katika utekelezaji wa miradi hiyo ni pamoja na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), TARURA, DUWASA, TANESCO, TTCL, TEMESA, e-GA, TPDC, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)". Amesema
Amesema Majengo na miundombinu hiyo imebuniwa kwa kuzingatia dhana ya Mji Janja (Smart City), ikizingatia matumizi ya nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua, uendelezaji wa mji wa kijani, mipango miji na uhifadhi wa mazingira.
"Majengo ya awamu ya pili yamegawanyika katika aina nne za miundo kulingana na mahitaji ya watumishi, ambapo baadhi yana uwezo wa kuchukua watumishi 300, 500, 1,400 na wengine takribani 150". Amesema Prof. Kabudi
Mbali na majengo, Prof. Kabudi amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1, ambazo zinatarajiwa kuimarisha usafirishaji, mawasiliano na upatikanaji wa huduma ndani na nje ya Mji wa Serikali.
Aidha, Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu mingine ikiwemo umeme wa chini ya ardhi wenye urefu wa kilomita 42, mifumo ya maji safi na maji taka, TEHAMA, CCTV, vituo vya zimamoto pamoja na mpango wa upandaji miti na uboreshaji wa mandhari ya Mji wa Serikali.
"Hatua hizo zinaifanya Mtumba kuwa zaidi ya eneo la majengo ya Serikali, bali kuwa sehemu ya uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuongeza ufanisi wa Serikali, kuboresha mazingira ya kazi na kuchochea fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla". Amesema Prof. Kabudi
Sambamba na Hayo, Prof. Kabudi amewaomba wananchi wa maeneo ya jirani, ikiwemo Mtumba, Mahoma Nyika, Ihumwa, Chamwino, Dodoma Mjini, UDOM na Hombolo, kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo ambao umetajwa kuwa sehemu ya historia ya maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba.
Uzinduzi huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa yatakayoonesha hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa azma ya kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha shughuli za Serikali.





Comments
Post a Comment