Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Mzee Stephen Masato Wasira, ameendelea kuonyesha dhamira yake ya kuhakikisha miradi ya maendeleo ya Chama inatekelezwa kwa ufanisi baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Kisasa ya CCM Wilaya ya Bunda, mkoani Mara.
Mradi huo ulioanza kutekelezwa mwezi Februari 2026 unagharimu zaidi ya shilingi milioni 700 na hadi sasa umefikia takribani asilimia 90 ya utekelezaji.
Ujenzi huo unasimamiwa na Ofisi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, huku ukilenga kujenga mazingira bora na ya kisasa yatakayorahisisha utekelezaji wa shughuli za Chama katika wilaya hiyo.
Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mzee Wasira amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi, lakini amesisitiza kuwa jambo muhimu zaidi ni kuhakikisha kazi zote zinazobaki zinakamilishwa kwa ubora wa hali ya juu na ndani ya muda uliopangwa.
"Ninatarajia ifikapo mwezi Agosti 2026 jengo hili liwe limekamilika kikamilifu, likiwa na viwango vya kisasa na ubora unaostahili. Lengo letu ni kuwa na ofisi itakayodumu kwa miaka mingi na kutoa mazingira mazuri ya kuwahudumia wanachama pamoja na wananchi," amesema Mzee Wasira.
Aidha, amesema ujenzi wa ofisi hiyo unaakisi dhamira ya CCM ya kuendelea kuimarisha miundombinu yake ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, uratibu wa shughuli za Chama na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Mara baada ya kukamilika, Ofisi hiyo ya Kisasa ya CCM Wilaya ya Bunda inatarajiwa kuwa moja ya majengo ya kisasa katika mkoa wa Mara, ikiwa ni alama ya maendeleo ya Chama na chachu ya kuimarisha utendaji kazi wa viongozi na watendaji wa CCM katika ngazi ya wilaya.













Comments
Post a Comment