NA: MWANDISHI WETU, DAR
Mkandarasi anayetekeleza mradi wa Maduka ya Biashara ya Maria Nyerere (Maria Nyerere Shopping Mall) ulio chini Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), amehimizwa kuongeza kasi ya ujenzi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, Julai 22, 2026, Jijini Dar es Salaam, katika ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UWT Taifa, kukagua uhai wa Chama na miradi ya Jumuiya hiyo.
Chatanda amesema, ipo haja ya mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi, huku akimshauri kuongeza wakandarasi wengine ili kumsaidia baadhi ya kazi na kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo.
"Mradi unakwenda vizuri, isipokuwa kwa mwenendo unavyokwenda na kwa muda tuliokubaliana huenda asikamilishe kwa wakati. Mkandarasi tunachomuhitaji aukamilishe mradi kwa mujibu wa tulivyokubaliana na kama kuna maeneo yeye hana uwezo wa kufanya, akabidhi kwa wakandarasi wengine (sub contractors) ili kazi ikamilike kwa wakati," amesema Chatanda.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti UWT Taifa, Zainabu Shomari, amesema mradi huo ni utekelezaji wa maagizo ya Chama wa kuzitaka Jumuiya zake kuwa na vitega uchumi.
"Chama kimeelekeza Jumuiya zake kujitegemea kiuchumi, kwahiyo, mradi huu ni utekelezaji wa maagizo na Chama na kwa hakika UWT tutafanikiwa kujitegemea," amesema Shomari.
Ikumbukwe kuwa, mradi wa Maria Nyerere Shopping Mall unatekelezwa eneo la Gerezani Jijini Dar es Salaam, ambapo unategemewa kuongeza mapato ili Jumuiya hiyo iwe na uwezo wa kuendesha shughuli zake bila kutegemea uwezeshwaji kutoka Chama ngazi ya Taifa.
Pamoja na mradi huo, Kamati hiyo, ilipata fursa ya kukagua eneo lake lenye ukubwa wa hekta 8.2, lililopo mtaa wa Zogo, kata ya Zingiziwa, wilayani Ilala, ambapo linategemewa kuongeza uwekezaji wa Jumuiya hiyo.








Comments
Post a Comment