📍Awaonya wajumbe wasifanye ushabiki wa Messi na Ronaldo
Na Mashaka Mhando, Muheza
MBUNGE wa Jimbo la Muheza ambaye pia ni Naibu Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma 'MwanaFA', amewataka wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo kutopepesa macho wala kubabaika linapokuja suala la kumchagua Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwakani.
MwanaFA ametoa kauli hiyo Leo Julai 23 wakati akizungumza na Wana-CCM wa kata za Kwakifua na Tingeni, ambapo ametumia jukwaa hilo kumpigia debe zito Mwenyekiti wa sasa wa mkoa huo, Ustadh Rajab Abdallah, akieleza kuwa rekodi ya kazi zake za kukijenga chama haijawahi kufikiwa na kiongozi yeyote nchini.
*Rekodi Zilizompa Kiki Ustadh Rajab*
Akijenga hoja ya kwanini wajumbe hawapaswi kufanya makosa, Mhe. Mwinjuma aliwataka wanachama hao kutaja mwenyekiti yeyote nchini aliyewahi kujenga nyumba za watumishi wa chama kila wilaya, ambapo wajumbe walijibu "hakuna."
"Hebu nitajieni Mwenyekiti yeyote aliyejenga nyumba za watumishi wa chama mkoa wowote hapa nchini? Alihakikisha nyumba hizo zinakwisha kila wilaya. Wabunge tulikuwa tukichanga lakini Mwenyekiti alichanga zaidi. Hapa Muheza amehakikisha tunajenga ofisi ya wilaya ya kisasa ya ghorofa, huyu hapaswi kukosa kura hata moja ya Wana-Muheza," alisema MwanaFA.
Aliongeza kuwa kazi zinazofanywa na Mwenyekiti huyo zimerahisisha sana utekelezaji wa majukumu ya chama na kuwaondolea mzigo wabunge, hivyo kuwapa nafasi nzuri ya kubaki na jukumu moja tu la kuwahudumia wananchi.
"Nyumba za watumishi zimekamilika, jengo letu linakwenda kwa kasi, na juzi tena Mwenyekiti huyo huyo katoa Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa mwingine wa chama. Hatuwezi kupata mwenyekiti kama Ustadh Rajab. Huyu ni mtu wa kumshikilia na kwenda naye katika uchaguzi," alisisitiza.
*"Hili Siyo Suala la Messi na Ronaldo, ni suala la uhai wa Chama chetu*
Katika kusisitiza uzito wa jambo hilo, MwanaFA alitumia lugha ya kimichezo kuonya wajumbe wasichukulie uchaguzi huo kama ushabiki usio na tija.
"Tunatakiwa watu wote tujijue tutamuunga mkono nani. Hili siyo suala la kubishania nani mkali kati ya Messi na Ronaldo; hili ni suala linalogusa maisha yetu, uhai wa chama chetu na mustakabali wake kwa kuwa na mtu muhimu kama yeye.
"Kwa hiyo watu wote tuhakikishe tunamlinda, Mungu akimpa uhai Mwenyekiti wetu, tuhakikishe tunaendelea naye atuongozee chama ngazi ya mkoa tunamchagua tena," alionya MwanaFA.
*Dua kwa Rais Samia*
Mwisho, Mbunge huyo aliwaomba wananchi wa Muheza kuendelea kumsomea dua na kumuombea afya njema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alisema Rais Samia ameutendea haki Mkoa wa Tanga na Wilaya ya Muheza kwa kupeleka fedha nyingi zilizowezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Samia, miradi mikubwa ya maji, elimu, na miundombinu ya barabara.






Comments
Post a Comment