_Dkt. Numbi atoa somo kutoka Ghana kuhusu usimamizi wa ushirikishwaji wa wazawa katika Sekta ya Madini_
📍MWANZA
Tume ya Madini imejipanga kuimarisha usimamizi wa ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini kwa kuhakikisha watoa huduma na wazalishaji wa bidhaa wanakidhi vigezo na viwango vya ubora vinavyohitajika, hatua inayolenga kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
Hayo yamesemwa leo, Julai 23, 2026, jijini Mwanza na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, kwenye Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF 2026), linalowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Dkt. Numbi amesema Tume itaendelea kuboresha usimamizi wa eneo la ushirikishwaji wa Watanzania ili kuhakikisha wananchi wanapata fursa zaidi za kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini, utoaji wa huduma, uzalishaji wa bidhaa na maeneo mengine ya mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini.
Akielezea uzoefu wa Ghana katika usimamizi wa ushirikishwaji wa wazawa, Dkt. Numbi amesema nchi hiyo imeweka mfumo madhubuti unaowataka waombaji wa fursa katika Sekta ya Madini kuwasilisha mipango ya ushirikishwaji wa wazawa, kulipa ada maalum na kurejesha sehemu ya fedha kwa Serikali kila mwisho wa mwaka.
Amesema mfumo huo pia unahakikisha watoa huduma wanakidhi vigezo vya kitaalamu na kuwa na uwezo unaohitajika kabla ya kupewa fursa ya kutoa huduma katika migodi ya madini.
Dkt. Numbi amewataka watoa huduma katika Sekta ya Madini kuhakikisha wanakidhi vigezo vinavyohitajika katika utoaji wa huduma na bidhaa migodini, sambamba na kuhakikisha bidhaa na huduma hizo zina ubora unaokidhi viwango vya juu.
“Ni muhimu kwa watoa huduma kuhakikisha wanakidhi vigezo vinavyohitajika na kutoa bidhaa na huduma zenye ubora unaokidhi viwango vya juu, kwa kuwa ubora ni msingi wa ushindani na uendelevu wa biashara katika Sekta ya Madini,” amesema Dkt. Numbi.
Aidha, amewataka Watanzania wanaoshiriki katika utoaji wa huduma na uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya migodi kuendelea kuimarisha uwezo wao, kuzingatia viwango vya ubora na kutumia teknolojia ili kuongeza ushindani na kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na Sekta ya Madini.
Jukwaa hilo, ambalo leo limefikia siku yake ya pili, linaendelea kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini, likiwemo suala la ushirikishwaji wa Watanzania katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), uzoefu bora kutoka kwa kampuni za Kitanzania zilizofanikiwa katika utekelezaji wa dhana ya ushirikishwaji wa Watanzania, pamoja na umuhimu wa kuzalisha rasilimaliwatu wenye ujuzi unaoendana na ukuaji wa teknolojia mpya katika Sekta ya Madini.
Vilevile, mdahalo maalum unajadili ajira, mafunzo na uhawilishaji wa teknolojia kama kichocheo cha kuongeza ushiriki na ujumuishaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, sambamba na utekelezaji wa mipango ya urithishaji wa nafasi za kazi, changamoto zinazojitokeza na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Jukwaa la LCCF 2026 limewakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini, wakiwemo makampuni ya uchimbaji wa madini, watoa huduma migodini, wafanyabiashara wa madini, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi, pamoja na vyama vya wachimbaji wa madini nchini.
Jukwaa hilo linafanyika chini ya kaulimbiu: “Kutoka Majadiliano hadi Utekelezaji: Kujenga Sekta Imara ya Madini kupitia Ushirikishwaji wa Watanzania na Uanzishwaji wa Viwanda.”









Comments
Post a Comment