Na Allan Kitwe, Tabora
WAKURUGENZI wa Halmashauri zote Mkoani Tabora wametakiwa kuchukua hatua stahiki kwa Mkandarasi au Mtaalamu yeyote atakayebainika kukwamisha utekelezaji miradi ya maendeleo inayogharamiwa na serikali katika maeneo yao.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha kupitia kwa Katibu Tawala (RAS) Dkt John Mboya alipokuwa akiongea na Wakuu wa Disivison na Vitengo, Watendaji na Madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Tabora.
Ameeleza kuwa serikali ya Awamu ya Sita imeleta fedha nyingi sana katika Mkoa huo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa soko kuu na stendi mpya ya kisasa Mjini Tabora, miradi hii ni muhimu sana.
‘Miradi yote inayotekelezwa hapa Tabora tunataka itekelezwe kwa weledi na ufanisi mkubwa, na thamani ya fedha ionekane kwa kila mradi, katika hili mkandarasi au msimamizi yeyote atakayezembea, atakiona cha moto', ameeleza.
RC amesisitiza kuwa wanataka kwenda na kasi ya viwango katika suala zima la utekelezaji shughuli za maendeleo hivyo akaagiza Wakurugenzi kuchukua hatua mara moja dhidi ya wakandarasi au mtalaamu yeyote anayekwamisha miradi.
Aidha ameonesha kusikitishwa na vibanda vya biashara vilivyojengwa katika halmashauri ya manispaa Tabora kukaa muda mrefu bila kutumika na kusababisha hasara ya zaidi ya milioni 47, hivyo akaagiza vianze kutumika mara moja.
‘Ili kwenda na kasi ya viwango, tunataka kila Mtumishi au Mtendaji abadilike, hatutaki kufanya kazi kwa mazoea, na kila halmashauri iandae mpango kazi wa kufanikisha utekelezaji majukumu yake na kila mtumishi ahusike’, ameongeza.
Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ghullam-Hussein Dewj ameunga mkono maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na kubainisha kuwa yamelenga kuchochea kais ya maendeleo katika halmashauri ya manispaa hiyo.
Amesisitiza kuwa maelekezo ya Mkoa ni maazimio, hivyo kazi yao ni moja tu kufanyia kazi yale yote yaliyosemwa katika kikao hicho ili kuharakisha utekelezaji miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.





Comments
Post a Comment