Mfanyabiashara Maarufu Nchini, Otieno Olunga Igogo, ameeleza namna alivyoguswa kufuatia kifo cha shemeji yake, Dkt. Alex Seka Odemba, aliyefariki dunia katika Jimbo la Michigan nchini Marekani siku chache zilizopita.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mzee Igogo amesema kuwa familia imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo hicho, akieleza kuwa marehemu alikuwa nguzo muhimu ya familia, mtu mwenye busara, upendo na aliyekuwa mstari wa mbele kuimarisha mshikamano wa ndugu na jamaa.
Aidha, Igogo ameeleza kuwa hakuna aliyedhani kuwa Dkt. Odemba angefariki katika kipindi ambacho alikuwa akijiandaa kufunga maisha yake nchini Marekani na kurejea Tanzania kuanza makazi mapya ambapo amesema siku moja kabla ya safari yake, marehemu alianza kujisikia vibaya kutokana na homa ya ghafla na kukimbizwa hospitalini, ambapo baadaye alifariki dunia.
Pia, Ameongeza kuwa taarifa za msiba huo ziliishtua familia na marafiki waliokuwa wakiamini kuwa wangempokea Tanzania ndani ya muda mfupi. Badala yake, walijikuta wakianza maandalizi ya kuupokea mwili wake kwa ajili ya mazishi.
Licha ya majonzi makubwa yaliyoikumba familia, Mzee Igogo amesema wameamua kuendelea kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu, wakitambua kuwa maisha ya mwanadamu yako chini ya mapenzi yake na hakuna anayeweza kubadili yaliyoamuliwa.
Kuhusu taratibu za mazishi, amesema mwili wa Dkt. Alex Seka Odemba unatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, siku ya Jumamosi Julai 25, 2026. Baada ya hapo utapelekwa Hospitali ya Lugalo kuhifadhiwa kabla ya kusafirishwa kwenda Kijiji cha Buturi, Wilaya ya Rorya mkoani Mara, ambapo mazishi yanatarajiwa kufanyika Alhamisi, Julai 30, 2026.
Familia imewaomba ndugu, jamaa, marafiki na wote waliomfahamu marehemu kuendelea kuwaombea katika kipindi hiki kigumu huku ikiendelea na maandalizi ya safari ya mwisho ya kumpumzisha Dkt. Alex Seka Odemba.
Dkt. Alex Seka Odemba atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika taasisi mbalimbali kwa umahiri wake na ubunifu kazini na iman iliyotukuka katika kulijenga taifa la Tanzania.


Comments
Post a Comment