DC LUBELA APONGEZA UZALENDO WA FORTUNATUS MAGAMBO, ARIDHISHWA NA UJENZI WA MADARASA MATANO SHULE YA MSINGI RING'WANI
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Wakili Angelina Marco Lubela, ameonyesha kuridhishwa kwake na ubora wa ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa katika Shule ya Msingi Ring'wani, iliyopo Kijiji cha Nyamatare, Kata ya Nyamatare, huku akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Fortunatus Makore Magambo, kwa moyo wake wa kizalendo na kujitolea kuunga mkono maendeleo ya elimu nchini.
Mhe. Lubela ametoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya mradi huo, uliofadhiliwa na Magambo kwa lengo la kusaidia Serikali kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, pamoja na kuondoa changamoto ya uhaba na uchakavu wa vyumba vya madarasa uliokuwa ukiikabili shule hiyo kwa muda mrefu.
Akizungumza baada ya ukaguzi, Mkuu huyo wa Wilaya amesema ameridhishwa na kiwango cha ubora wa ujenzi huo, akieleza kuwa madarasa hayo yamejengwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya wanafunzi na walimu, na kwamba yatakuwa chachu ya kuinua kiwango cha taaluma katika shule hiyo.
"Nimeridhishwa sana na ubora wa mradi huu. Huu ni mfano wa uzalendo na moyo wa kujitolea unaopaswa kuigwa na wadau wengine wa maendeleo. Tunamshukuru sana Ndugu Fortunatus Magambo kwa kuamua kurejesha sehemu ya mafanikio yake kwa jamii kupitia sekta ya elimu," amesema Mhe. Lubela.
Amesema mchango huo unaunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuboresha miundombinu ya elimu nchini, sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 inayolenga kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Mhe. Lubela amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwathamini na kushirikiana na wadau binafsi wanaojitokeza kusaidia maendeleo ya jamii, akibainisha kuwa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Aidha, amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha miradi yenye tija inaendelea kutekelezwa katika Kata ya Nyamatare na Wilaya ya Serengeti kwa ujumla, hususan katika sekta za elimu, afya na huduma nyingine za kijamii.
Kwa upande wake, wananchi wa Kijiji cha Nyamatare wameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo, wakisema utamaliza adha ya wanafunzi kusomea katika madarasa yasiyokuwa salama na yenye msongamano mkubwa. Wamesema kukamilika kwa madarasa hayo kutaboresha mazingira ya kujifunzia, kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kuifanya Shule ya Msingi Ring'wani kuwa miongoni mwa shule zenye miundombinu bora katika eneo hilo.
Mradi huo ni sehemu ya mchango wa kijamii wa Fortunatus Makore Magambo, unaolenga kusaidia maendeleo ya jamii kupitia uwekezaji katika sekta ya elimu. Hatua hiyo imepongezwa na viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, wakieleza kuwa ni mfano bora wa ushirikiano unaohitajika ili kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Ziara hiyo ya ukaguzi ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi, akiwemo Diwani wa Kata ya Nyamatare Mhe. Mzee Maheke, Katibu wa CCM Kata ya Nyamatare Nyamahemba Moturi, Mtendaji wa Kata Maria Joram, pamoja na viongozi wengine wa chama na Serikali waliofuatilia maendeleo ya mradi huo.



Comments
Post a Comment