Akiuliza swali bungeni, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa, alitaka kujua ni lini Serikali itajenga Madaraja ya Nyasaungu na Tuguti yaliyopo katika barabara ya Musoma Busekela, ambayo ni miongoni mwa barabara muhimu za kiuchumi katika Wilaya ya Musoma Vijijini.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo katika kukuza shughuli za kiuchumi na kurahisisha usafiri wa wananchi wa eneo hilo.
Mhandisi Kasekenya amesema tayari zabuni ya ujenzi wa kilomita 40 za barabara hiyo imeshatangazwa, huku madaraja ya Nyasaungu na Tuguti yakitengwa na mradi huo ili yajengwe kwa utaratibu maalum utakaochochea utekelezaji wake kwa haraka zaidi.
"Tunafahamu barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa wananchi, na madaraja hayo ni muhimu. Serikali inaendelea na taratibu za kuyajenga pamoja na utekelezaji wa kilomita 40 za barabara ambayo tayari imeshatangazwa," amesema Mhandisi Kasekenya.
Ujenzi wa madaraja hayo unatarajiwa kuimarisha mawasiliano, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma, pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Musoma Vijijini na Mkoa wa Mara kwa ujumla.




Comments
Post a Comment