Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Tharman Shanmugaratnam, amewasili nchini Tanzania kwa ziara ya Kiserikali ya siku tatu kuanzia Juni 8 hadi 10, 2026.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Rais Tharman Shanmugaratnam akiwa ameambatana na mkewe, Bi. Jane Ittogi Shanmugaratnam, alipokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb), pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Peter Ulanga.
Ziara hii ya Kiserikali ni ya kwanza kufanywa na Rais wa Singapore nchini Tanzania tangu mataifa hayo mawili yalipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1980.
Ziara hiyo inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Singapore.
Wakati wa ziara yake, Rais Tharman atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ikulu ya Dar es Salaam. Viongozi hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi yatakayolenga kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, uchumi wa kidijitali, maendeleo ya bandari, elimu, maendeleo ya ujuzi, utalii na miundombinu.
Ziara hiyo pia itahusisha ushiriki katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Tanzania na Singapore pamoja na ziara visiwani Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Ziara hiyo ya Kiserikali inatarajiwa kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi na kuimarisha zaidi ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Singapore kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo mawili.















Comments
Post a Comment