Na Mwandishi wetu Jovina Massano.
Ushirikiano wa Wadau wa utalii, wananchi na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi mlima Kilimanjaro.
Kauli hii imetolewa na Viongozi mara baada kuripotiwa kuzuka moto ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.
Septemba 5,2026 Waziri wa maliasili na Utalii,Dkt. Ashatu Kijaji(Mb) amewasili na kutembelea eneo ulipozuka moto ndani ya hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.
Lengo la kutembelea eneo hilo ni kuona hali ya eneo hilo pamoja na hatua zinazochukuliwa kudhibiti na kuzima moto huo.
Dkt. Kijaji amesema kuwa moto huo umedhibitiwa kwa asilimia 90 na shughuli za Utalii zinaendelea vizuri ndani ya hifadhi hiyo huku akitoa rai kwa wananchi wanaozunguka hifadhi za Taifa kuepuka shughuli zinazoweza kusababisha moto.
"Wananchi wanapaswa kuzingatia mipaka iliyowekwa kati yao na maeneo hifadhi na kuepuka shughuli zinazoweza kusababisha moto na kupelekea kuleta athari kwa mazingira na wanyamapori ndani ya hifadhi",amesema Dkt.Kijaji.
Hata hivyo Kamishna wa uhifadhi wa TANAPA Massana Mwishawa amebainisha kuwa zoezi la kuzima na kudhibiti moto huo linaendelea vizuri.
Udhibiti huo umefanyika chini ya Ushirikiano wa Jeshi la uhifadhi,Jeshi la Zimamoto na uokoaji pamoja na wadau mbalimbali wa Utalii huku hatua za kuhakikisha moto huo unadhibitiwa kikamilifu zikiendelea.
Aidha shukrani zimetolewa na Kamishna Msaidizi wa uhifadhi na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano TANAPA, Catherine Mbena kwa wadau wote walishiriki na kuweka jitihada za kudhibiti moto huo na kutambua mchango wao wa hali na mali katika kushiriki na kujitolea kulinda rasilimali za hifadhi.
Amesisitiza Ushirikiano wa wananchi wanaozunguka hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro,wadau wa Utalii na TANAPA kwa kuwa ni muhimu katika kuimarisha uhifadhi na kukabiliana na majanga kwa kulinda rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadae.





Comments
Post a Comment