Na Angela Sebastian, Ngara
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Ngara mjini, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Magereza–Kabalenzi kwa kiwango cha lami utarahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kwenda sokoni, hatua wanayoamini itachochea shughuli za kiuchumi na kuongeza kipato cha wananchi pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 0.55 imejengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Ngara kwa gharama ya zaidi ya Shilingi milioni 316. Mbali na kuboresha mandhari ya mji, wananchi wameitaja kuwa ni fursa muhimu ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, ikiwemo mazao yanayopelekwa katika nchi jirani ya Burundi hivyo kuongeza mzunguko wa biashara katika eneo hilo.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Ngara, Mhandisi Mokoro Magori, akisoma taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa mbio za mwenge Kitaifa 2026a amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Oktoba 2024 na unalenga kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na kubadili mandhari ya mji.
Amesema kukamilika kwa barabara hiyo pia kutapunguza vumbi lililokuwa likiwakabili wakazi na wafanyabiashara wa eneo hilo, sambamba na kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa.
Kwa upande wa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu, Wazo Mwang’onda, amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa lengo la kuboresha hadhi ya miji, kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara ya barabara na vyombo vya moto, pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Aidha, ameupongeza TARURA kwa kazi nzuri ya kujenga barabara zenye viwango na kuwataka wananchi kutunza miundombinu hiyo ili idumu na kuendelea kuwanufaisha.
Kwa upande wao, wananchi wa mitaa ya Mulugwanza Kati na Ngara mjini ambako mradi huo unapatikana, Benasia Zachali, Dishoni Bwakunga na Manase Ntiluvako, wamemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo, wakisema barabara hiyo ni ya thamani kubwa kwao. Wamesema imekuwa msaada kwa wananchi, hususani wale wanaoishi maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Burundi, ikiwemo Mugoma, kwa kuwa inarahisisha usafirishaji wa mazao kuja kuuzwa Ngara na hivyo kuongeza kipato cha wakulima.
Katika Wilaya ya Ngara, Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zimepita katika miradi saba yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.8, ikiwemo miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha huduma na kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.






Comments
Post a Comment