MTWARA
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma, amehitimisha rasmi mashindano ya soka ya 'CRDB Nanauka Cup 2026' yaliyokuwa sehemu ya tamasha kubwa la Mtwara Festival, huku Naliendele FC ikiibuka kidedea na kutwaa ubingwa.
Katika fainali hiyo ya kusisimua iliyopigwa Julai 18 2026 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara, Naliendele FC iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penati dhidi ya Vigaeni FC baada kutoshana nguvu kwa sare ya 1-1 na kufanikiwa kukabidhiwa kombe, medali, na kitita cha shilingi milioni tatu. Vigaeni FC iliyoshika nafasi ya pili iliondoka na medali pamoja na shilingi milioni mbili, huku mshindi wa tatu akijinyakulia shilingi milioni moja.
Mashindano haya yameandaliwa na kuratibiwa na Mbunge wa Mtwara Mjini ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana, Mhe. Dkt. Joel Arthur Nanauka. Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri Mwinjuma amewapongeza waandaaji kwa kufikia asilimia 100 ya malengo yao, hasa kwa kufanikiwa kuibua vijana 20 wenye vipaji ambao watakabidhiwa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kuendelezwa.
Ligi hiyo iliyodumu kwa mwezi mmoja ilishirikisha timu 18 kutoka kata zote za jimbo la Mtwara Mjini, ambapo jumla ya mechi 52 zilichezwa.













Comments
Post a Comment