Benki ya Azania imeidhinisha gawio la jumla ya shilingi bilioni 18.36 katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Wanahisa (AGM) uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro.
Gawio hilo la shilingi 98.62 kwa kila hisa linawakilisha asilimia 30 ya faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 61.4 ambayo Benki ilipata katika mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2025, ikionesha dhamira ya Benki ya Azania kuendelea kutoa thamani endelevu kwa wanahisa wake na kujenga msingi imara wa ukuaji kwa miaka ijayo.
Mkutano huo uliwakutanisha Wanahisa, Wajumbe wa bodi, menejimenti, Wadhibiti pamoja na wadau mbalimbali kujadili utendaji wa Benki na mwelekeo wake wa kimkakati, jambo linaloendelea kuonesha imani kubwa ya wawekezaji katika mustakabali wa taasisi hiyo.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Eng.Julius B. Ndyamukama - Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Azania alisema kuwa uamuzi wa kutoa gawio hilo unaakisi uimara wa kifedha wa Benki pamoja na dhamira yake ya kuendelea kuongeza thamani kwa wanahisa.
Katika mkutano huo, wanahisa pia walipatiwa taarifa kuhusu mafanikio ya kimkakati ya Benki, ikiwemo kuendelea kupanua mtandao wa matawi, kuimarisha huduma za kidijitali, kuongeza uwezeshwaji wa biashara ndogo na za kati (SMEs), sekta ya kilimo, pamoja na huduma za kifedha zinazolenga wanawake na vijana sambamba na uwekezaji katika kuboresha huduma kwa wateja.
Benki ya Azania inaendelea kuthibitisha kuwa benki imara ya kizawa nchini Tanzania, ikiwa na msingi madhubuti wa wanahisa unaojumuisha mifuko ya hifadhi ya jamii kama Mfuko wa Hifadhi kwa Jamii ya Watumishi wa Umma(PSSSF),Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) pamoja na wanahisa wadogo wakiwemo wafanyakazi wa Benki.
Benki ya Azania itaendelea kuimarisha utendaji wake sokoni, kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania huku ikiendelea kuongeza thamani kwa wadau wake wote.








Comments
Post a Comment