Jumla ya Watanzania 440 wameondoka kwa hiari kutoka maeneo mbalimbali nchini Afrika Kusini na kurejea Tanzania, huku Watanzania 192 wakiondoka Jijini Cape Town leo, Septemba 4, 2026, kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, amesema Watanzania hao 192 wanatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo saa nne usiku.
Amesema idadi hiyo inafanya jumla ya Watanzania 267 kutoka Cape Town pekee kuwa wameondoka na kurejea Tanzania ndani ya siku mbili, baada ya Watanzania 75 kuondoka jana, Septemba 3, 2026.
Watanzania hao 267 wanaungana na Watanzania 173 waliosafirishwa kutoka Durban Agosti 26, 2026, hivyo kufikisha jumla ya Watanzania 440 waliosafiri kwa hiari kutoka Afrika Kusini kurejea Tanzania hadi Septemba 4, 2026.
Balozi Bwana amewatakia Watanzania hao safari njema na maisha mema wanaporejea katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.




Comments
Post a Comment