Na Angela Sebastian
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwango’nda, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa kuhakikisha majukwaa ya vijana yanashushwa kutoka ngazi ya wilaya hadi kata, vijiji na mitaa, ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata elimu na taarifa kuhusu fursa zinazotolewa na Serikali.
Mwango’nda alitoa agizo hilo wakati akizindua Jukwaa la Vijana katika Wilaya ya Kyerwa, akieleza kuwa majukwaa hayo yamekuwa yakifanya kazi katika ngazi ya wilaya, hivyo ni muhimu viongozi na watendaji wa Halmashauri kuyapeleka karibu zaidi na vijana walioko katika maeneo yao. Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wa vijana kuhusu fursa mbalimbali, ikiwemo mikopo na programu za kuwawezesha kiuchumi.
“Serikali imeweka nguvu nyingi kwa vijana, na hamasa ya sasa ni kuhakikisha vijana wanajiajiri kupitia vikundi mbalimbali. Serikali iko tayari kuwahangaikia; kinachopungua kwa sasa ni elimu na namna ya kutumia fursa zilizopo. Hivyo viongozi wa Halmashauri wanapaswa kujiongeza na kuwafikia huko huko walipo,” alisema Mwango’nda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Vijana katika Kongamano la Vijana la Wilaya ya Kyerwa, jumla ya vijana 1,244 kutoka kata 24 wamekwishafikiwa na fursa za mikopo kupitia mpango wa asilimia 10 unaotolewa na Halmashauri. Afisa huyo alisema fursa hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha vijana kuongeza mitaji ya biashara na shughuli zao za uzalishaji, hatua inayosaidia kuinua uchumi wa familia zao.
Katika ziara hiyo ya Mwenge wa Uhuru, Kiongozi huyo pia alizindua mradi wa kikundi cha vijana cha Umoja wa Mafundi Nyamiyaga, ambacho kimenufaika na mkopo wa Shilingi milioni 61. Mradi huo ni miongoni mwa mifano ya namna mikopo inayotolewa kupitia Halmashauri inavyoweza kuwa chachu ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kuendesha shughuli za kiuchumi kwa pamoja.
Mwenyekiti wa vijana wa kikundi hicho, Yusto Rutahananwa, alisema Serikali imeendelea kuwaunga mkono katika shughuli zao, ikiwemo kuwapatia mashine za kuchomelea zenye thamani ya Shilingi milioni 1.5. Alisema vifaa hivyo vimeongeza uwezo wa kikundi kufanya shughuli za ufundi na kutoa huduma kwa jamii, huku vikifungua zaidi fursa za ajira na kipato kwa vijana.
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Zaitun Msofe, alisema Halmashauri itaendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali. Alisema mkakati huo utaenda sambamba na kuhakikisha huduma na elimu kwa vijana zinawafikia wananchi hadi ngazi ya vijiji, ili kijana asiye katika makao ya wilaya naye aweze kupata taarifa na kutumia fursa zilizopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.




Comments
Post a Comment