Njedengwa, Dodoma
Serikali imeongeza kasi ya mapinduzi ya sekta ya kilimo kwa kuanza kusambaza pampu za umwagiliaji na kuchimba visima 390 katika mikoa 15, hatua inayolenga kuwawezesha wakulima kulima mwaka mzima, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Mpango huo unatarajiwa kunufaisha wakulima 15,022 waliounganishwa katika vikundi 769, huku ekari 13,518.75 zikiingizwa kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwainua wakulima wadogo, hususan wanawake na vijana, kwa kuwapatia uhakika wa maji kwa ajili ya uzalishaji.
Alisema pamoja na kuendelea na ujenzi wa miradi mikubwa na ya kimkakati ya umwagiliaji, Serikali imeamua kuwekeza pia katika uchimbaji wa visima na usambazaji wa pampu kwa vikundi vya wakulima ili kuongeza tija mashambani.
"Tumeelekezwa kutafuta njia zitakazowawezesha wananchi wa kipato cha chini kujiongezea kipato. Ndiyo maana pamoja na miradi mikubwa ya umwagiliaji, tumeanza uchimbaji wa visima na ugawaji wa pampu kwa wakulima wadogo," alisema Mndolwa.
Alieleza kuwa pampu hizo zinalenga kuwasaidia wakulima wanaolima karibu na mito na maziwa kufanya kilimo chenye tija bila kutegemea mvua.
Kwa mujibu wa Mndolwa, Serikali imenunua pampu 2,000, ambapo pampu 1,000 tayari zimepokelewa na kusambazwa katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Kigoma, Simiyu, Geita na Katavi kwa ajili ya kuanza kutumika.
Alisema wanufaika wa awamu hiyo ni wanawake 6,335 na wanaume 8,702, ambao kwa pamoja wataongeza uzalishaji na kipato kupitia kilimo cha umwagiliaji.
"Pampu hizi zitawasaidia wakulima kuondokana na utegemezi wa mvua na kuwawezesha kulima misimu yote ya mwaka, jambo litakaloongeza uzalishaji na kipato chao," alisema.
Mndolwa alisema hadi sasa Serikali imechimba visima 390 katika mikoa 15, huku Dodoma ikiongoza kwa visima 93, ikifuatiwa na Manyara na Tabora zenye visima 44 kila mmoja, Geita 42, Singida 32, Njombe 30, Tanga 22, Iringa 20, Mara na Morogoro visima 17 kila mmoja.
Mikoa mingine iliyonufaika ni Pwani na Arusha zenye visima 10 kila mmoja, Mtwara nane, Mbeya saba na Ruvuma visima vitano.
Aidha,
Amesema Serikali imeanza ununuzi wa pampu 500 kwa ajili ya visima hivyo, ambapo pampu 100 tayari zimepokelewa, nyingine 100 ziko njiani kutoka kwa mtengenezaji na pampu 300 zipo katika hatua za mwisho za manunuzi.
Mbali na hilo, Serikali inatarajia kupokea pampu nyingine 1,000 zinazotumia nishati ya jua zitakazosambazwa katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa umeme, hatua itakayopanua zaidi huduma za umwagiliaji nchini.
Mndolwa alifafanua kuwa visima vinachimbwa kwenye mashamba ya vikundi vya wakulima lakini vinabaki kuwa mali ya umma ili kuhakikisha wanachama wote wanapata huduma kwa usawa na miundombinu hiyo inadumu kwa muda mrefu.
Aliongeza kuwa vikundi vyote vinavyonufaika husajiliwa kwa mujibu wa sheria ili kuimarisha usimamizi wa miradi na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Kwa mujibu wa Mndolwa, utekelezaji wa mpango huo pia unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 4,000 kwa vijana watakaoshiriki katika ufungaji, uendeshaji na usimamizi wa mifumo ya umwagiliaji.
Alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuifanya sekta ya umwagiliaji kuwa nguzo ya mapinduzi ya kilimo, kuongeza usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi.











Comments
Post a Comment