Na Mwandishi Wetu, Mbeya
MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomon Itunda, amewatunuku vyeti wahitimu 70 wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (KAPS) na kuwataka kutumia elimu waliyoipata kuwa chachu ya mabadiliko chanya na kutengeneza fursa za kujiajiri badala ya kusubiri ajira za kuajiriwa.
Hafla hiyo ya mahafali imefanyika Julai 17, 2026, katika viwanja vya chuo hicho kilichopo mtaa wa Forest, Jijini Mbeya, ambapo wahitimu hao walihitimisha masomo yao na kutunukiwa Astashahada (Certificate) ya Maendeleo ya Jamii.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo akiwa kama Mgeni Rasmi, Mhe. Itunda aliwapongeza wahitimu hao kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu waliouonesha katika kipindi chote cha masomo yao, na kuwakumbusha kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea nguvu kazi yenye maarifa na uzalendo.
"Mnapaswa kwenda kuwa chachu ya maendeleo katika maeneo yenu kwa kuzingatia misingi ya kazi na utu. Tumieni elimu mliyoipata hapa kujiajiri na kuajiri wengine, huku mkizingatia maadili ya kazi, uzalendo na uwajibikaji katika kuwahudumia wananchi," alisisitiza Mhe. Itunda.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya alitumia jukwaa hilo kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa na maboresho yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya elimu.
Alibainisha kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye miundombinu ya vyuo, imeongeza upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia, na inaendelea kuwalipa walimu stahiki zao mbalimbali kwa wakati ili kuongeza ufanisi na morali katika utoaji wa elimu nchini.
Mahafali hayo, yaliyohitimishwa kwa kaulimbiu ya “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele” kama msisitizo wa mchango wa wahitimu kuijenga jamii, yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wahadhiri, wadau wa maendeleo, pamoja na wazazi na walezi waliojitokeza kushuhudia vijana wao wakihitimu.





Comments
Post a Comment