MSTAHIKI MEYA MANISPAA YA KIBAHA AWATAKA WAZAZI KUIMARISHA NA KUBORESHA ELIMU KWA KUSHIRIKIANA NA WALIMU
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dr Nicas Mawazo amewataka wazazi wa Shule zilizopo Manispaa ya Kibaha kuiga jitihada zinazofanywa na Shule zingine katika kuimarisha na kuboresha elimu kwenye Shule zao kwa kushirikiana na walimu.
Hayo ameyasema wakati wa kikao na Kamati ya Shule ya Sekondari ya Mwambisi, iliyofika katika Ofisi ya Mstahiki Meya kwa ajili ya kujadiliana na masuala mbalimbali.
Akizungumza baada ya Kamati hiyo kuwasilisha mapendekezo yao, Mstahiki Meya Dr Nicas ameipongeza Kamati hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wanafunzi wa Shule yaSekondari Mwambisi wanaendelea kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
"Nawapongeza sana Kamati ya Shule kwa jitihada kubwa mnazofanya , Shule zingine wangekuwa wanafuata utaratibu huu ina maana tungekuwa tunafanya vizuri zaidi na zipo baadhi ya Shule zinafanya hivyo na matokeo yao yanakuwa ni mazuri," amesema Dr Nicas.
Ameongeza kuwa,, Ofisi ya Mstahiki Meya itaongezea hela ya ununuzi wa mashine ya Photocopy ambapo iliyokuwepo awali imeharibika na kusababisha wanafunzi kushindwa kupata fursa ya kufanya mitihani mara kwa mara kutokana na gharama.
"Ofisi yangu itachangia kiasi cha Tshs 1,500,000/ = kwa ajili ya ununuzi wa Photocopy ili wanafunzi 1080 waliopo katika Shule ya Sekondari Mwambisi iweze kuwasaidia,"amesema Dr Nicas
Aidha, Mstahiki Meya amesema Manispaa ya Kibaha imejipanga katika kuhakikisha inajenga miundombinu ya kutosha kwa ajili ya wanafunzi wapya na hivyo amewaasa wanafunzi na wazazi kulinda miundo mbinu hiyo ili wanafunzi wengine waje kuitumia.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Sekondari Mwambisi, Bw. Hamza Omari Duruge amemshukuru Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha kwa kukubali kuonana nao pamoja na kuchangia kiasi cha Tshs 1,500,000/= kwa ajili ya ununuzi wa Mashine ya photocopya ambayo iliyokuwepo imeharibika.
Duruge amesema, jambo hilo ni kubwa sana na wao kama Kamati ya Shule wataendelea kusimamia jitihada zinazofanywa na wazazi za kuhakikisha Shule ya Sekondari Mwambisi inaendelea kufanya vizuri kwenye mitihani yake inayokuja kwa kidato cha pili na kidato cha nne.
Katika kikao hicho, Mstahiki Meya ametoa rai kwa wazazi wote kuwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeendelea kujenga shule za nsingi na sekondari na Halmashauri inatoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundo mbinu ya Shule ikiwemo madawati ya wanafunzi na ukarabati wa baadhi ya majengo.




Comments
Post a Comment