SERIKALI imefafanua kuwa makadirio ya Shilingi bilioni 730 yanayotajwa katika Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El-Niño si fedha zilizotengwa na Serikali kwa matumizi ya moja kwa moja, bali ni makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutekeleza mpango huo kwa kushirikisha Serikali, taasisi, sekta binafsi, mashirika ya kitaifa na kimataifa pamoja na wadau wengine.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema mpango huo umeandaliwa kufuatia utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wa Agosti 18, 2026, uliotabiri uwepo wa El-Niño yenye nguvu inayoweza kusababisha mvua kubwa, mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya mlipuko kwa binadamu na wanyama pamoja na madhara kwa miundombinu, makazi na shughuli za kiuchumi.
Amesema mpango huo umeandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri, mashirika ya kitaifa na kimataifa, Umoja wa Mataifa na Asasi zisizo za Kiserikali, kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Maafa.
Kwa mujibu wa Prof. Kabudi, makadirio ya Shilingi bilioni 730 yamezingatia ukubwa wa madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na El-Niño ya mwaka 2026/27, uchambuzi wa madhara kwa sekta mbalimbali pamoja na uzoefu wa madhara yaliyosababishwa na matukio ya El-Niño ya miaka ya 2023/24, 2015/16 na 1997/98.
“Fedha zilizotengwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli hizo kwa sekta zote ni Shilingi bilioni 10,” amesema Prof. Kabudi, akisisitiza kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 730 ni makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutoka kwa wadau mbalimbali katika kutekeleza shughuli zilizoainishwa kwenye mpango.
Amesema baadhi ya shughuli hizo tayari zinaendelea kutekelezwa na sekta na wadau mbalimbali kupitia bajeti zao za mwaka wa fedha 2026/27, kulingana na vipaumbele vya kuzuia na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Mpango huo umejikita katika ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ikiwemo barabara, madaraja, reli, mitaro, makalvati pamoja na miundombinu ya afya, elimu, usafiri, nishati ya umeme, maji safi, maji taka na mawasiliano katika maeneo hatarishi.
Aidha, Serikali imepanga kuimarisha hifadhi ya akiba ya chakula, kuhakikisha vifaa vya uokoaji na misaada ya kibinadamu vinapatikana katika maghala ya kikanda, kuandaa maeneo salama ya makazi ya muda na kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kuzuia na kupunguza madhara ya mafuriko, radi, maporomoko ya ardhi na magonjwa ya mlipuko.
Serikali pia imeagiza maeneo hatarishi yatambuliwe mapema, tathmini za vihatarishi zifanyike na wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi wahamasishwe kuhamia maeneo salama endapo kutakuwa na tishio la maafa.
Katika sekta ya afya, mifugo na kilimo, mamlaka zimeelekezwa kuandaa mipango ya kuzuia milipuko ya magonjwa kwa binadamu, wanyama na mimea.
Wizara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zimeagizwa kufanya ukaguzi na kuimarisha miundombinu muhimu, hususan madaraja, makalvati na mitaro, huku usimamizi wa mazingira ukiimarishwa kwa kudhibiti taka ngumu, kusafisha njia za maji na kuimarisha kingo za mito na mabwawa.
Serikali pia imewataka wananchi kutumia fursa ya mvua hizo kwa shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, ufugaji, uvunaji wa maji na uvuvi, huku wakitumia mbinu bora za kilimo na kuchagua mazao pamoja na mbegu zinazofaa kwa msimu wa Vuli.
Prof. Kabudi ametoa wito kwa vyombo vya habari na wadau wote kutoa taarifa sahihi kuhusu mpango huo ili kuondoa taharuki na kusaidia jamii kuelewa hatua zinazochukuliwa kabla, wakati na baada ya kutokea kwa majanga.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu, kupitia maelekezo yaliyotolewa Agosti 26, 2026, imewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote ambayo kwa mujibu wa utabiri inaweza kuathiriwa na mvua za El-Niño kuchukua hatua za maandalizi na kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza.
Aidha, wananchi wametakiwa kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kwa wakati pindi maafa yanapotokea.
“Usimamizi wa maafa ni jukumu letu sote, shiriki sasa na chukua hatua,” amesisitiza Prof. Kabudi.




Comments
Post a Comment