Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby, amekabidhi pikipiki 370 kwa vijana wa Jimbo la Gairo kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kujenga vyanzo vyao vya kipato.
Akizungumza katika hafla ya kiwakabidhi pikipiki hizo 370, Mbunge huyo wa Jimbo la Gairo Shabiby amesema pikipiki hizo zimetolewa kwa kuzingatia zaidi vijana wenye uhitaji na wasio na uwezo wa kuanzia, akisisitiza kuwa umaskini ni miongoni mwa vigezo vilivyozingatiwa katika kuwafikia wanufaika.
Amesema mpango huo utaendelea, ambapo kila mwisho wa mwezi vikundi vitano vitapatiwa pikipiki 50 kwa mfumo wa mkopo, huku akieleza kuwa mpango huo unalenga kuwafikia vijana wengi zaidi ndani na nje ya Gairo.
Shabiby amewataka vijana waliopatiwa pikipiki hizo kuzitumia kwa uangalifu, kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati, akisema uaminifu wao ndio utakaowezesha vijana wengine kupata fursa hiyo.
“Ninyi mliochukua pikipiki si kwamba ndiyo mwisho kupata pikipiki. Ninyi sasa ni mabalozi wazuri. Mtakapolipa vizuri, ndipo mtakapopewa pikipiki,” amesema Shabiby.
Aidha, amesema pikipiki hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuimarisha shughuli za kiuchumi Gairo, hususan kilimo, ambacho amesema kinaendelea kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya uchumi wa wananchi wa jimbo hilo.
Amesema Gairo imekuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji wa mazao yanayosafirishwa na kutumika katika maeneo mbalimbali, hivyo uwezeshaji wa vijana kupitia vyombo vya usafirishaji ni sehemu ya kuwaunganisha na fursa za kiuchumi.
Mbunge huyo pia amewataka wanufaika kuepuka uzembe na kuendesha pikipiki kwa usalama, akisisitiza kuwa mafanikio ya mpango huo yanategemea namna vijana watakavyotumia fursa walizopewa.
“Tunawaomba mjendeshe kwa heshima… fanyeni bidii. Hakuna tajiri yoyote aliyefanikiwa bila kufanya kazi,” amesema.
Amesema lengo la mpango huo si kuwapatia vijana pikipiki pekee, bali kuwajengea uwezo wa kuwa na shughuli endelevu za kiuchumi, kuongeza kipato na hatimaye kuwawezesha vijana wengine kupata fursa kama hizo.



Comments
Post a Comment