Na Angela Sebastian, Bukoba
MWENGE wa Uhuru mwaka 2026 umekagua na kupongeza mradi wa vijana 47 wanaojishughulisha na ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, unaotekelezwa na vikundi saba katika Kata ya Kemondo, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.
Mradi huo upo chini ya programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT-Uvuvi), inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kupitia sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026, Wazo Mwang’onda, alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuwawezesha vijana kupitia miradi ya kiuchumi, huku akiipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Alisema Serikali imeendelea kuhakikisha vikundi vinavyonufaika vinapatiwa nyenzo za kazi, mafunzo kwa vitendo, mikopo yenye masharti nafuu pamoja na pembejeo zinazohitajika katika shughuli za uvuvi na ufugaji wa samaki.
“Tumeukagua mradi huu na kuona kuwa ni mzuri, kwani vizimba vya kufugia samaki vinavyomilikiwa na vijana vinaendelea kuzalisha na kuwawezesha kujipatia kipato, hivyo kuwasaidia kujikwamua na umaskini,” alisema Mwang’onda.
Aliongeza kuwa Serikali imekusudia kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwekeza katika miundombinu ya huduma za kijamii pamoja na miradi mbalimbali inayowawezesha wananchi kiuchumi na kuongeza fursa za ajira na kipato.
Akizungumza kuhusu manufaa ya mradi huo, Katibu wa kikundi cha BBT-Uvuvi, Yusuph Hiliyai, alisema mtaji walioupata kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba umewawezesha kuendesha shughuli za ufugaji wa samaki kwa ufanisi.
Alisema mradi huo umehusisha upatikanaji wa vizimba 47, pembejeo za uvuvi pamoja na boti moja, ambavyo kwa pamoja vimegharimu zaidi ya Sh bilioni 1.1 na kuwa chachu ya vijana hao kujikwamua kiuchumi na kuongeza kipato.
Hiliyai alisema kila kizimba kina uwezo wa kuhifadhi vifaranga 11,280 vya samaki na kwamba baada ya miezi saba wanatarajia kuvuna takribani tani 4.28 za samaki kwa kila kizimba.
Alisema mavuno hayo yanatarajiwa kuwa na thamani ya Sh milioni 32.1 kwa kila kizimba, jambo ambalo linaonesha fursa kubwa ya kiuchumi iliyopo katika ufugaji wa samaki kwa kutumia teknolojia ya vizimba.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Fatna Raay, alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri hiyo ilitoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni 573.8 kwa vikundi 51 vya vijana vinavyojishughulisha na kilimo, mifugo, ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba pamoja na biashara.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuwawezesha vijana kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ili kuongeza uzalishaji na kujenga uchumi endelevu.
Kwa ujumla, Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 umepitia miradi sita yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4.8 katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, ikiwa na lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Miradi hiyo imejikita katika sekta za elimu, afya, maji, viwanda, utawala bora na uwezeshaji wananchi kiuchumi, ikiwemo ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Katangalala, Mradi wa Maji Bumai, ujenzi wa Ofisi ya Kata ya Karabagaine, kiwanda cha kuchakata parachichi, mradi wa vijana wa ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa.






Comments
Post a Comment