Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema taasisi hiyo imeendelea kutumia teknolojia za kisasa na akili unde katika kuboresha huduma za upasuaji, uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa.
Akizungumza leo, Septemba 1, 2026, Dkt. Ulisubisya amesema MOI inatumia teknolojia inayochakata taarifa za mgonjwa na kutengeneza ramani maalum inayomwongoza daktari wakati wa upasuaji, hivyo kumwezesha kufika kwa usahihi katika eneo lenye tatizo na kupunguza hatari wakati wa matibabu.
Amesema teknolojia hiyo pia imeanza kutumika katika uchukuaji wa sampuli za uvimbe kwa ajili ya uchunguzi wa maabara, ambapo vifaa vidogo humsaidia daktari kufikia eneo lenye tatizo na kuchukua sampuli bila kulazimika kufanya upasuaji mkubwa kama ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa Dkt. Ulisubisya, matumizi ya teknolojia hiyo yamewezesha kupunguza ukubwa wa afua, muda wa mgonjwa kukaa hospitalini na kuongeza ufanisi wa huduma za uchunguzi na matibabu.
Kuhusu matatizo ya pingili za mgongo, amesema MOI imeboresha huduma kwa kutumia mitambo ya kisasa inayowezesha madaktari kufanya matibabu kupitia sehemu ndogo, ikiwemo kuweka vifaa maalum vinavyosaidia kurejesha mpangilio na mfumo wa pingili za mgongo bila kufungua eneo kubwa kama ilivyokuwa hapo awali.
Aidha, amesema MOI imeanzisha huduma maalum ya kudhibiti maumivu sugu (Chronic Pain), ambayo ni miongoni mwa huduma za kisasa zinazolenga kuwasaidia wagonjwa wenye maumivu ya muda mrefu. Amesema wataalamu wamepatiwa mafunzo maalum na tayari huduma hiyo imeanza kuonyesha matokeo mazuri kwa wagonjwa.
Dkt. Ulisubisya pia amesema MOI imeendelea kutoa huduma maalum kwa wagonjwa wenye viungo vilivyopooza kutokana na kuathirika kwa mishipa ya fahamu au kuharibika kwa misuli baada ya kupata majeraha, kwa kutumia mbinu za kitabibu zinazowezesha kurejesha uwezo wa sehemu zilizoathirika.
Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hizo ni sehemu ya juhudi za MOI kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora, salama, sahihi na zenye kupunguza muda wa matibabu hospitalini.











Comments
Post a Comment