Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeadhimisha miaka 62 tangu kuanzishwa kwake Septemba 1, 1964, huku maadhimisho hayo yakifanyika sambamba na kufungwa kwa Wiki ya Sita ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia ya Majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Viwanja vya Gofu vya Lugalo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Jacob John Mkunda, amesema historia ya JWTZ imejengwa kupitia utekelezaji wa majukumu ya kulinda taifa pamoja na kushiriki katika shughuli zinazogusa maisha ya wananchi.
Jenerali Mkunda amesema JWTZ limeendelea kuimarisha uwezo wa askari wake ili kukabiliana na majukumu mbalimbali ya kitaifa, huku misingi ya uzalendo, weledi na uwajibikaji ikiendelea kuwa sehemu ya utendaji wa jeshi hilo.
Kwa mujibu wa Jenerali Mkunda, maadhimisho hayo yamekuja wakati ambapo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea kutafuta njia za kuongeza ushirikiano wa majeshi yao, si katika masuala ya kijeshi pekee bali pia katika shughuli zinazolenga kusaidia jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Sita ya Ushirikiano wa Majeshi ya Afrika Mashariki 2026, Brigedia Jenerali Dkt. Agatha Mary Katua, amesema programu hiyo imewezesha wanajeshi wa nchi mbalimbali kukutana, kufanya kazi kwa pamoja na kubadilishana uzoefu.
Amesema Tanzania, Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda na Somalia ziliwakilishwa na timu zilizoshiriki katika shughuli za kijamii zilizolenga kuwafikia wananchi katika maeneo ya Dar es Salaam, Pwani na Zanzibar.
Brigedia Jenerali Dkt. Katua amesema moja ya mafanikio yaliyopatikana ni utoaji wa huduma za afya bila malipo, ambapo jumla ya wananchi 11,749 walihudumiwa katika vituo saba, huku shughuli nyingine zikihusisha misaada kwa makundi yenye mahitaji maalumu na maboresho ya baadhi ya miundombinu.
Akieleza kuhusu msingi wa programu hiyo, Dkt. Katua amesema wazo la kuanzishwa kwa Wiki ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia lilitokana na mapendekezo ya Kikundi Kazi cha Wataalamu wa Ulinzi katika Michezo na Utamaduni kilichokutana mwaka 2016.
Aidha, amesema JWTZ linaona ushirikiano huo kama njia ya kuendeleza uhusiano wa karibu kati ya majeshi na wananchi, huku likieleza utayari wa kuendelea kushirikiana na nchi wanachama wa EAC katika utekelezaji wa shughuli za kijeshi na kiraia. Kabla ya shughuli hizo kuanza, kamati iliyokuwa ikiongozwa na Dkt. Katua iliratibu maandalizi yaliyomuwezesha Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Salum Haji Othman, kuzindua rasmi wiki hiyo.






Comments
Post a Comment