Na Mwanamkuu Mwandoro,Tanga.
Wananchi mkoani Tanga wametakiwa kuchukua tahadhari kubwa kufuatia mvua zinazotarajiwa kunyesha na kutopuuzia utabiri wa hali ya hewa kwani kuna uwezekano wa kunyesha kwa mvua kubwa katika msimu ujao wa mvua, huku kukiwa na dalili za kuwepo kwa hali ya hewa ya El Niño.
Angalizo hilo limetolewa na Meneja wa Mamlaka ya Hali ya Hewa mkoa wa Tanga Kurwa Mbwambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alizitaka pia kamati za maafa kuzingatia taarifa za hali ya hewa na kuchukua tahadhari mapema.
Aidha Mbwambo aliongeza kuwa viashiria vya hali ya hewa vinaonesha uwepo wa hali ya El Niño ambayo inaweza kuathiri mwendo wa mvua katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba utabiri wa sasa unaonesha kuwepo kwa mvua za vipindi vifupi,na huku mvua za vuli zikitarajiwa kuanza kunyesha katika juma la kwanza/pili la mwezi oktoba 2026 hadi Januari 2027.
“Wananchi wasipuuze taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa sababu zinatolewa ili kuwawezesha kuchukua hatua za tahadhari na kulinda maisha pamoja na mali zao,” alisema Mbwambo.
Mbwambo pia amewataka wananchi kuhakikisha wanasafirisha mifareji na mitaro ili kuruhusu maji kupita kwa pindi chote Cha mvua kwani Kwa kufanya hiyo itasaidia pia kupunguza athari za mvua/ mafuriko katika maeneo yao.
Sambamba na hayo pia Mbwambo amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika vifaa vya utabiri wa hali ya hewa pamoja na wataalamu umeboresha usahihi wa utabiri, ambapo kwa sasa utabiri wa hali ya hewa unafikia kiwango cha makadirio cha asilimia 94 cha usahihi.
Kwa mujibu wake, TMA tayari imewasilisha taarifa za kina za utabiri kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote pamoja na mamlaka za wilaya, zikiwemo taarifa zinazoonyesha namna kila wilaya inavyoweza kuathiriwa na mvua hizo zinazotarajiwa.
Mbwambo aliwataka wananchi wanaoishi mabondeni na maeneo mengine yaliyo katika hatari ya mafuriko kuchukua tahadhari mapema badala ya kusubiri hadi mvua kubwa zianze kunyesha.
TMA imeeleza kuwa ingawa mvua za Vuli zinatarajiwa rasmi kuanza mwezi Oktoba katika maeneo mengi, baadhi ya maeneo nchini yanaweza kuanza kupata mvua mapema kuanzia Septemba 2026
Mamlaka hiyo pia imeonya kuwa hali ya El Niño kuelekea mwishoni mwa mwaka inaweza kusababisha msimu wa mvua unaoanza Novemba 2026 hadi Aprili 2027 kuanza mapema katika baadhi ya maeneo ambayo kwa kawaida hupata msimu mmoja mkuu wa mvua kwa mwaka.
Hata hivyo, TMA imesisitiza kuwa utabiri wa msimu hutoa mwelekeo wa hali ya hewa kwa maeneo mapana na vipindi vya miezi mitatu. Kwa hiyo, mabadiliko ya muda mfupi katika mwenendo wa mvua yataendelea kufuatiliwa kupitia utabiri wa muda wa kati na mfupi.

Comments
Post a Comment