Na Mwanamkuu Mwandoro,Tanga
Serikali mkoani Tanga imetoa agizo Kwa wamiliki wote wa Mabasi yanayosafirisha abiria kwenda nje ya mkoa,nchi jirani na maeneo mbalimbali ya nchi kuhakikisha kuwa ifikapo September 8,2026 Magari yote yanaanza na kumaliza safari zake katika kituo kikuu cha Mabasi kilichopo Kange.
Agizo hilo linatokana na maadhimio yaliyotolewa na ofisi ya Waziri mkuu, Kamati ya Bunge inayoshughulika na Ofisi ya Rais tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa 'TAMISEMI' pamoja na wamiliki na wadau wa usafirishaji kwa lengo la kuhakikisha huduma ya usafirishaji inaimarika pamoja na kuchangia maendeleo ya mkoa huo hususani kwa Halmashauri ya jiji la Tanga kupitia kituo hicho ambacho kinatarajia kuwa kitovu cha uchumi.
Akizungumza katika kikao cha pamoja na wadau wa usafirishaji wakiwemo wamiliki wa Mabasi Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani amesema kuwa utekelezaji wa agizo hilo umezingatia utekelezaji wa Sheria ndogo ya Halmashauri 'by laws' ya mwaka 2019 huku akiitaka Halmashauri kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote wa usafirishaji.
"Baada ya kupitia mapendekezo na ushauri ulioyotolewa na wadau wa usafirishaji na viongozi mbalimbali kwa kuzingatia Sheria ndogo ya Halmashauri 'by laws' ya mwaka 2019 Magari yote yatapaswa kuanza na kumaliza safari zake katika kituo kikuu cha Mabasi Kange wamiliki wote wanapaswa kuzingatia Sheria hizi na tumekubaliana suala hili lianze rasmi tarehe 8,2026" amesema Dkt Buriani.
Amesema kuwa agizo hilo limeambatana na mapendekezo ambayo yanatakiwa kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuitaka mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini 'LATRA' kuanzisha njia za safari za Daladala zinazotoka maeneo mbalimbali ya jiji kwenda Moja Kwa Moja katika kituo hicho cha Kange, kuwepo kwa gari la Zimamoto na uokoaji, kukaguliwa kwa vituo vyote vya Mabasi vilivyopo katikati ya jiji kama vinakidhi vigezo.
Kwaupande wake Ismail Masoud Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga, alisema wamepokea maelekezo lakini alitaka mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau yafanyiwe kazi na vikao vya Kila mwezi vifanyiwe kazi,
"Tunaomba mapendekezo yote na maboresho yaliyotolewa na wadau mbalimbali wakiwemo abiria na wamiliki wa mabasi na Daladala tunaomba yafanyiwe kazi" Aliongeza Masoud
Aidha kabla ya kutekelezwa kwa agizo hilo Balozi Dkt. Buriani ameiagiza Halmashauri ya jiji la Tanga kuhakikisha kuwa katika kituo hicho kunakuwa na maeneo maalumu kwaajili ya maegesho la Daladala, Bodaboda, Magari binafsi na kuweka mabango ili kuwarahisishia abiria na wananchi kuweza kuendelea na safari .



Comments
Post a Comment