MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, amesema chuo hicho kinaendelea kuweka mkazo katika utafiti, ubunifu, sayansi na teknolojia ili kutatua changamoto za jamii na kuchangia maendeleo ya taifa.
Prof. Chibunda amesema hayo leo, Agosti 31, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Idara ya Habari MAELEZO jijini Dodoma, akieleza kuwa SUA kwa sasa inatekeleza miradi 172 ya utafiti kwa kushirikiana na taasisi na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Amesema tafiti hizo zinagusa maeneo mbalimbali yakiwemo kilimo, mifugo, afya, uvuvi, misitu, rasilimali maji, mabadiliko ya tabianchi na masoko ya mazao, huku zikilenga kuongeza tija, kuboresha maisha ya wananchi na kutoa ushahidi wa kusaidia Serikali katika sera na mipango ya maendeleo.
Katika kilimo, amesema SUA imefanya tafiti za mbegu zinazostahimili ukame, wadudu na magonjwa, pamoja na uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na mimea, lishe na udhibiti wa visumbufu vya mazao na mifugo. Pia, chuo kinafanya tafiti za chanjo, tiba na mbinu bora za ufugaji, uvuvi na uzalishaji wa viumbe maji.
Katika afya, Prof. Chibunda amesema SUA inashirikiana na zaidi ya hospitali 80 nchini katika tafiti za utambuzi wa Kifua Kikuu (TB), ikiwemo matumizi ya panya waliofunzwa kitaalamu kupitia APOPO kubaini vimelea vya TB. Panya hao pia hutumika katika kugundua mabomu ya ardhini na kusaidia kubaini nyara za Serikali.
Amesema SUA imetumia takribani miaka 25 katika kuwafundisha na kuwazalisha panya hao, na sasa imeingia makubaliano na TAWA kuwawezesha kutumika katika maeneo ya mipakani, viwanja vya ndege na bandarini kusaidia kudhibiti usafirishaji haramu wa nyara kama pembe za ndovu na magamba ya kakakuona.
Akizungumzia mafanikio hayo, Prof. Chibunda amemtaja Magawa, panya aliyefunzwa na APOPO na kutumwa Cambodia, aliyesaidia kugundua mabomu 71 ya ardhini na mabaki 38 ya vilipuzi, huku akichangia kusafisha zaidi ya mita za mraba 141,000 za ardhi. Kwa heshima ya mchango wake, SUA imeipa moja ya barabara zake jina la Magawa Road, huku kumbukumbu yake ikiendelea kuenziwa.
Aidha, amesema SUA inafanya utafiti wa kutumia bundi aina ya Barn Owl kudhibiti panya waharibifu mashambani bila kutegemea sumu za kemikali, pamoja na kutumia harufu bandia zinazofanana na za wanyama wanaowinda panya ili kuwazuia kuharibu mazao. Teknolojia hiyo pia inatafitiwa kusaidia kupunguza migogoro kati ya binadamu, mifugo na wanyamapori.
Katika ubunifu na hakimiliki, Prof. Chibunda amesema SUA imefanikiwa kupata hataza 16 za kimataifa, zikiwemo zinazohusu mbegu mpya zinazostahimili ukame, uzalishaji wa miche kwa njia ya tissue culture, pamoja na teknolojia za lishe, chanjo na tiba dhidi ya visumbufu vya mazao na mifugo.
Prof. Chibunda amesisitiza kuwa tafiti za SUA hazipaswi kubaki maabara au kwenye vitabu, bali zinapaswa kuzalisha suluhisho zinazotumika moja kwa moja kuboresha maisha ya wananchi, kuongeza uzalishaji, kulinda mazingira na kusaidia Serikali kufanya maamuzi yenye ushahidi.
Ametoa wito kwa waandishi wa habari kuendelea kuelimisha jamii kuhusu mafanikio ya tafiti hizo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza na kutunza historia ya ubunifu huo, ikiwemo mchango wa panya kama Magawa.
Tafiti za SUA zinaendelea kuunganisha elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu katika kutafuta suluhisho za changamoto za kilimo, afya, mifugo, mazingira, uhifadhi wa wanyamapori na matumizi endelevu ya rasilimali kwa maendeleo ya Taifa.



Comments
Post a Comment