RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na uhamisho wa Wakuu wa Mikoa pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, mabadiliko hayo yanahusisha uteuzi wa Wakuu wapya wa Mikoa minne, uhamisho wa Wakuu wa Mikoa sita pamoja na mabadiliko katika nafasi za Makatibu Tawala wa Mikoa.
Wakuu wapya wa Mikoa
Katika uteuzi huo, CP. Salum Rashid Hamduni, aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Alexander Pastory Mnyeti ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, huku Stanslaus Haroon Nyongo akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Aidha, Jumanne Abdallah Sagini ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Wakuu wa Mikoa waliohamishwa
Kwa upande wa uhamisho, Martine Reuben Shigela amehamishwa kutoka Mkoa wa Geita na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara.
Said Mohamed Mtanda amehamishwa kutoka Mwanza kwenda Simiyu, akichukua nafasi ya Anamringi Macha ambaye amestaafu.
Abubakar Mussa Kunenge amehamishwa kutoka Pwani kwenda Songwe, akichukua nafasi ya Jabiri Omari Makame, ambaye atapangiwa majukumu mengine.
Vilevile, Beno Moris Malisa amehamishwa kutoka Mbeya kwenda Tabora, akichukua nafasi ya Paul Matiko Chacha, ambaye aliteuliwa kuwa Katibu wa NEC, Idara ya Oganaizesheni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Adam Kighoma Malima amehamishwa kutoka Morogoro kwenda Lindi, akichukua nafasi ya Zainab Telack, ambaye amestaafu.
Kwa upande mwingine, Queen Cuthbert Sendiga amehamishwa kutoka Manyara kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Makatibu Tawala nao wabadilishwa
Katika nafasi za Makatibu Tawala wa Mikoa, Richard Marcellino Kayombo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani.
Aidha, Balandya Mayuganya Elikana amehamishwa kutoka Mwanza kwenda Mbeya.
Dkt. Fatuma Ramadhan Mganga amehamishwa kutoka Singida kwenda Mwanza, huku Pili Hassan Mnyema akihamishwa kutoka Pwani kwenda Shinyanga.
Rodrick Lazaro Mpogolo naye amehamishwa kutoka Mbeya kwenda kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uapisho wa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wateule utafanyika katika tarehe ambayo itapangwa baadaye.
Mabadiliko hayo yanatarajiwa kuleta sura mpya katika uongozi wa mikoa husika, huku viongozi hao wakipewa majukumu ya kuendelea kusimamia utekelezaji wa mipango na shughuli za Serikali katika maeneo yao.

Comments
Post a Comment